Skip to content
Mwanzo 33:1-11

Mwanzo 33:1-11

1
Yakobo akainua macho akamwona Esau akija na watu wake 400, kwa hiyo akawagawanya watoto kati ya Lea, Raheli na wale watumishi wake wawili wa kike.
2
Akawaweka wale watumishi wa kike na watoto wao mbele, Lea na watoto wake wakafuata, Raheli na Yosefu wakaja nyuma.
3
Yeye mwenyewe akatangulia mbele na kusujudu mara saba alipomkaribia ndugu yake.
4
Lakini Esau akamkimbilia Yakobo kumlaki na kumkumbatia, akamwangukia shingoni na kumbusu. Nao wakalia.
5
Esau akainua macho akawaona wale wanawake na watoto. Akauliza, “Hawa uliofuatana nao ni nani?” Yakobo akamjibu, “Ni watoto ambao Mungu amempa mtumishi wako kwa neema.”
6
Kisha wale watumishi wa kike na watoto wao wakakaribia na kusujudu.
7
Kisha Lea na watoto wake wakaja na kusujudu. Mwisho wa wote wakaja Yosefu na Raheli, nao pia wakasujudu.
8
Esau akauliza, “Una maana gani kuhusu makundi hayo yote niliyokutana nayo?” Akasema, “Ni ili kupata kibali machoni pako, bwana wangu.”
9
Lakini Esau akamwambia, “Ndugu yangu, tayari nina wingi wa mali. Ulivyo navyo viwe vyako mwenyewe.”
10
Yakobo akasema, “La hasha! Tafadhali, kama nimepata kibali machoni pako, upokee zawadi hii kutoka kwangu. Kwa maana kuuona uso wako, ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa takabali kubwa.
11
Tafadhali ukubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options