Skip to content
Mwanzo 27:20-38

Mwanzo 27:20-38

20
Isaki akamuuliza mwanawe. “Umepataje haraka namna hii, mwanangu?” Akajibu, “Bwana Mungu wako amenifanikisha.”
21
Kisha Isaki akamwambia Yakobo, “Mwanangu tafadhali sogea karibu nami ili nikupapase, nione kama hakika ndiwe Esau mwanangu, au la.”
22
Yakobo akasogea karibu na baba yake Isaki, ambaye alimpapasa na kusema, “Sauti ni ya Yakobo, bali mikono ni ya Esau.”
23
Hakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na nywele kama ya ndugu yake Esau, kwa hiyo akambariki.
24
Akamuuliza, “Hivi kweli wewe ni mwanangu Esau?” Akajibu, “Mimi ndiye.”
25
Kisha akasema, “Mwanangu, niletee sehemu ya mawindo yako nile, ili nipate kukubariki.” Yakobo akamletea naye akala, akamletea na divai akanywa.
26
Kisha Isaki baba yake akamwambia, “Njoo hapa, mwanangu, unibusu.”
27
Kwa hiyo akamwendea akambusu. Isaki aliposikia harufu ya nguo zake, akambariki, akasema, “Aha, harufu ya mwanangu ni kama harufu ya shamba ambalo Bwana amelibariki.
28
Mungu na akupe umande kutoka mbinguni na utajiri wa duniani: wingi wa nafaka na divai mpya.
29
Mataifa na yakutumikie na mataifa yakusujudie. Uwe bwana juu ya ndugu zako, na wana wa mama yako wakusujudie. Walaaniwe wale wakulaanio, nao wale wakubarikio wabarikiwe.”
30
Baada ya Isaki kumaliza kumbariki na baada tu ya Yakobo kuondoka kwa baba yake, ndugu yake Esau akaingia kutoka mawindoni.
31
Naye pia akaandaa chakula kitamu akamletea baba yake. Kisha akamwambia, “Baba yangu, keti ule sehemu ya mawindo yangu, ili upate kunibariki.”
32
Isaki baba yake akamuuliza, “Wewe ni nani?” Akajibu, “Mimi ni mwanao, mzaliwa wako wa kwanza, Esau.”
33
Isaki akatetemeka kwa nguvu sana, akasema, “Alikuwa nani basi, ambaye aliwinda mawindo akaniletea? Nilikula kabla tu hujaja na nikambariki, naye hakika atabarikiwa!”
34
Esau aliposikia maneno haya ya baba yake, akalia sauti kubwa na ya uchungu, na kumwambia baba yake, “Nibariki mimi, mimi pia, baba yangu!”
35
Lakini akasema, “Ndugu yako amekuja kwa udanganyifu na akachukua baraka yako.”
36
Esau akasema, “Si ndiyo sababu anaitwa Yakobo? Amenidanganya mara hizi mbili: Alichukua haki yangu ya kuzaliwa na sasa amechukua baraka yangu!” Kisha akauliza, “Hukubakiza hata baraka moja kwa ajili yangu?”
37
Isaki akamjibu Esau, “Nimemfanya yeye kuwa bwana juu yako, pia nimewafanya ndugu zako wote kuwa watumishi wake, nimemtegemeza kwa nafaka na divai mpya. Sasa nitaweza kukufanyia nini, mwanangu?”
38
Esau akamwambia baba yake, “Je, baba yangu una baraka moja tu? Unibariki mimi pia, baba yangu!” Kisha Esau akalia kwa sauti kubwa.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options