Mwanzo 24:15-27
15
Ikawa kabla hajamaliza kuomba, Rebeka akatokea akiwa na mtungi begani mwake. Alikuwa binti wa Bethueli. Bethueli alikuwa mwana wa Milka aliyekuwa mke wa Nahori ndugu wa Abrahamu.
16
Huyu msichana alikuwa mzuri sana wa sura, bikira, ambaye hakuna mtu aliyekuwa amekutana naye kimwili. Aliteremka kisimani, akajaza mtungi wake akapanda juu.
17
Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye akamwambia, “Tafadhali nipe maji kidogo katika mtungi wako.”
18
Yule msichana akasema, “Kunywa, bwana wangu.” Akashusha kwa haraka mtungi mkononi mwake na akampa, akanywa.
19
Baada ya kumpa yule mtumishi yale maji, akamwambia, “Nitateka maji kwa ajili ya ngamia zako pia mpaka wote watosheke.”
20
Akafanya haraka kumimina maji kwenye birika ya kunyweshea wanyama, akakimbia kisimani kuteka maji mengine na akateka ya kuwatosha ngamia wake wote.
21
Pasipo kusema neno, yule mtumishi akamtazama kwa makini aone kama Bwana ameifanikisha safari yake, au la.
22
Ikawa ngamia walipokwisha kunywa wote, yule mtumishi akampa huyo msichana pete ya puani ya dhahabu yenye uzito wa beka moja na bangili mbili za dhahabu zenye uzito wa shekeli kumi.
23
Kisha akamuuliza, “Wewe ni binti wa nani? Tafadhali uniambie, je, kuna nafasi katika nyumba ya baba yako tutakapoweza kulala?”
24
Yule msichana akamjibu, “Mimi ni binti wa Bethueli, mwana wa Milka aliyemzalia Nahori.”
25
Akaendelea kusema, “Kwetu kuna majani mengi na malisho, tena kuna nafasi kwa ajili yenu kulala.”
26
Yule mtumishi akasujudu na kumwabudu Bwana,
27
akisema, “Atukuzwe Bwana, Mungu wa bwana wangu Abrahamu, ambaye hakuondoa wema na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mimi nami, Bwana ameniongoza safarini akanifikisha nyumbani kwa jamaa za bwana wangu.”
Settings