Skip to content
Ezekieli 46:6-24

Ezekieli 46:6-24

6
Siku ya mwezi mwandamo atatoa fahali mchanga, wana-kondoo sita na kondoo dume, wote wasiwe na dosari.
7
Atatoa kuwa sadaka ya nafaka efa moja pamoja na fahali mmoja, efa moja na kondoo dume mmoja na pamoja na wana-kondoo kama atakavyo kutoa, pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.
8
Wakati mkuu anayetawala aingiapo, atapitia kwenye baraza ya njia ya lango, naye atatoka nje kwa njia hiyo hiyo.
9
“ ‘Wakati watu wa nchi wanapokuja mbele za Bwana katika sikukuu zilizoamriwa, yeyote aingiaye kwa lango la kaskazini kuabudu atatoka nje kwa lango la kusini na yeyote aingiaye kwa lango la kusini atatoka nje kwa lango la kaskazini. Hakuna mtu yeyote atakayerudi kwa kupitia lango lile aliloingilia, lakini kila mmoja atatoka nje kwa lango linalokabili lile aliloingilia.
10
Mkuu anayetawala atakuwa miongoni mwao, akiingia nao ndani wanapoingia, naye atatoka nao nje wanapotoka.
11
“ ‘Kwenye sikukuu na kwenye sikukuu zilizoamriwa, sadaka ya nafaka itakuwa efa moja pamoja na fahali mmoja, efa moja pamoja na kondoo dume mmoja, pamoja na idadi ya wana-kondoo kama mtu apendavyo kutoa, pamoja na hini ya mafuta kwa kila efa.
12
Mkuu anayetawala anapotoa sadaka ya hiari kwa Bwana, ikiwa ni sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya amani, lango linaloelekea mashariki litafunguliwa kwa ajili yake. Atatoa sadaka yake ya kuteketezwa au sadaka yake ya amani kama afanyavyo katika siku ya Sabato. Kisha atatoka nje, naye akiisha kutoka nje, lango litafungwa.
13
“ ‘Kila siku utamtoa mwana-kondoo wa mwaka mmoja asiyekuwa na dosari kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana, utaitoa kila siku asubuhi.
14
Pia kila siku asubuhi pamoja na hiyo sadaka utatoa sadaka ya nafaka, ikiwa na sehemu ya sita ya efa pamoja na theluthi moja ya hini ya mafuta ya kuchanganya na ule unga. Utoaji wa sadaka hii ya nafaka kwa Bwana ni amri ya daima.
15
Kwa hiyo mwana-kondoo na sadaka ya nafaka na mafuta vitatolewa kila siku asubuhi kwa ajili ya sadaka ya daima ya kuteketezwa.
16
“ ‘Hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Ikiwa mkuu atawalaye atatoa zawadi kutoka kwenye urithi wake na kumpa mmoja wa wanawe, hiyo zawadi itakuwa pia kwa wazao wake, itakuwa mali yao kwa urithi.
17
Hata hivyo, kama atatoa zawadi kutoka urithi wake na kumpa mmoja wa watumishi wake, mtumishi anaweza kuiweka mpaka mwaka wa uhuru, kisha itarudishwa kwa mkuu anayetawala. Urithi wake ni wa wanawe peke yao, ni mali yao.
18
Mkuu anayetawala hana ruhusa kuchukua urithi wowote wa watu na kuwaondoa kwenye mali zao. Mkuu atawalaye atawapa wanawe urithi wao, kutoka kwenye mali zake mwenyewe, ili kwamba pasiwe na mtu wangu yeyote atakayetengwa na urithi wake.’ ”
19
Kisha mtu yule akanileta kwa kupitia kwenye ingilio lililokuwa kando ya lango mpaka kwenye vyumba vitakatifu vinavyoelekea kaskazini, ambavyo ni vya makuhani, naye akanionyesha mahali fulani upande wa mwisho wa magharibi.
20
Akaniambia, “Mahali hapa ndipo makuhani watakapotokosea sadaka ya hatia na sadaka ya dhambi na kuoka sadaka ya nafaka, kuepuka kuzileta katika ukumbi wa nje na kushirikisha utakatifu kwa watu.”
21
Baada ya hapo akanileta kwenye ukumbi wa nje na kunizungusha kwenye pembe zake nne, nami nikaona katika kila pembe ya huo ukumbi kulikuwa na ukumbi mwingine.
22
Katika pembe nne za huo ukumbi wa nje kulikuwa na kumbi nyingine, zenye urefu wa dhiraa arobaini na upana wake dhiraa thelathini, ambapo hizo kumbi kwenye hizo pembe nne zilikuwa na vipimo vilivyo sawa.
23
Mzunguko wa ndani wa hizo kumbi nne ulikuwa na ukingo wa jiwe, zikiwa na sehemu zilizojengwa kwa ajili ya moto kuzunguka chini ya huo ukingo.
24
Akaniambia, “Hizi ndizo sehemu za kupikia ambazo wale wanaohudumu kwenye Hekalu watatokosea dhabihu za watu.”

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options