Ezekieli 34:23-31
23
Nitaweka juu yao mchungaji mmoja, mtumishi wangu Daudi, naye atawachunga, atawachunga na kuwa mchungaji wao.
24
Mimi Bwana nitakuwa Mungu wao, naye mtumishi wangu Daudi atakuwa mkuu miongoni mwao. Mimi Bwana nimenena.
25
“ ‘Nitafanya nao Agano la amani na kuwaondoa wanyama wa mwitu kutoka nchi yao ili kondoo wangu waweze kupumzika nyikani na msituni kwa salama.
26
Nitawabariki wao pamoja na maeneo yanayozunguka kilima changu. Nitawanyeshea mvua kwa majira yake, kutakuwepo mvua za baraka.
27
Miti ya shambani itatoa matunda yake na ardhi itatoa mazao yake, watu watakaa salama katika nchi yao. Watajua kuwa Mimi ndimi Bwana, nitakapovunja vifungo vya nira zao na kuwaokoa kutoka mikono ya wale waliowafanya watumwa.
28
Hawatatekwa tena nyara na mataifa, wala wanyama pori hawatawala tena. Wataishi kwa salama, wala hakuna yeyote atakayewatia hofu.
29
Nitawapa nchi yenye sifa kutokana na mazao yake, hawatapatwa na njaa katika nchi tena wala hawatadharauliwa na mataifa.
30
Ndipo watakapojua kuwa Mimi, Bwana, Mungu wao, niko pamoja nao, na kwamba wao, nyumba ya Israeli, ni watu wangu, asema Bwana Mwenyezi.
31
Ninyi ni kondoo wangu, kondoo wa malisho yangu, ninyi ni watu wangu, nami ni Mungu wenu, asema Bwana Mwenyezi.’ ”
Settings