Kutoka 8:1-22
1
Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.
2
Kama ukikataa kuwaruhusu kuondoka, basi nitaipiga nchi yako yote kwa kuwaletea vyura.
3
Mto Naili utafurika vyura. Watakuja kwenye jumba lako la kifalme na katika chumba chako cha kulala na kitandani mwako, katika nyumba za maafisa wako na kwa watu wako, vyura hao wataingia katika meko yenu na kwenye vyombo vya kukandia unga.
4
Vyura watapanda juu yako, juu ya watu wako na maafisa wako wote.’ ”
5
Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyoosha mkono wako ukiwa na ile fimbo yako juu ya vijito, mifereji na madimbwi, fanya vyura waje juu ya nchi ya Misri.’ ”
6
Ndipo Aroni akaunyoosha mkono wake juu ya maji ya Misri, nao vyura wakatokea na kuifunika nchi.
7
Lakini waganga wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao, nao pia wakafanya vyura kuja juu ya nchi ya Misri.
8
Ndipo Farao akamwita Mose na Aroni na kusema, “Mwombeni Bwana awaondoe vyura kutoka kwangu na kwa watu wangu, nami nitawaachia watu wenu waende kumtolea Bwana dhabihu.”
9
Mose akamwambia Farao, “Ninakupa heshima ya kuamua ni wakati gani wa kukuombea wewe, maafisa wako na watu wako ili kwamba vyura watoke kwenu na kwenye nyumba zenu. Isipokuwa wale walio katika Mto Naili.”
10
Farao akasema, “Kesho.” Mose akamjibu, “Itakuwa kama unavyosema, ili upate kujua kwamba hakuna yeyote kama Bwana Mungu wetu.
11
Vyura wataondoka kwako na katika nyumba zako, kwa maafisa wako na kwa watu wako, ila watabakia katika Mto Naili tu.”
12
Baada ya Mose na Aroni kuondoka kwa Farao, Mose akamlilia Bwana kuhusu vyura aliokuwa amewaleta kwa Farao.
13
Naye Bwana akafanya lile Mose alilomwomba. Vyura wakafia ndani ya nyumba, viwanjani na mashambani.
14
Wakayakusanya malundo, nchi nzima ikanuka.
15
Lakini Farao alipoona pametokea nafuu, akaushupaza moyo wake na hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile Bwana alivyokuwa amesema.
16
Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyoosha fimbo yako uyapige mavumbi ya ardhi,’ nayo nchi yote ya Misri mavumbi yatakuwa viroboto.”
17
Wakafanya hivyo, Aroni aliponyoosha mkono wake wenye fimbo na kuyapiga mavumbi ya nchi, viroboto wakawajia watu na wanyama. Mavumbi yote katika nchi ya Misri yakawa viroboto.
18
Lakini waganga walipojaribu kutengeneza viroboto kwa siri ya uganga wao, hawakuweza. Nao viroboto walikuwa juu ya watu na wanyama.
19
Waganga wale wakamwambia Farao, “Hiki ni kidole cha Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukawa mgumu naye hakuwasikiliza, kama vile Bwana alivyosema.
20
Kisha Bwana akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi na usimame mbele ya Farao wakati anapokwenda mtoni nawe umwambie, ‘Hili ndilo Bwana asemalo: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.
21
Kama hutawaachia watu wangu waondoke nitakupelekea makundi ya mainzi juu yako, kwa maafisa wako, kwa watu wako na kwenye nyumba zenu. Nyumba za Wamisri zitajazwa mainzi, hata na ardhi yote ya Misri.
22
“ ‘Lakini siku ile nitafanya kitu tofauti katika nchi ya Gosheni, ambapo watu wangu wanaishi, hapatakuwepo na makundi ya mainzi, ili mpate kujua kwamba Mimi, Bwana, niko katika nchi hii.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings