Kumbukumbu 33:20-29
20
Kuhusu Gadi akasema: “Atabarikiwa yeye aongezaye milki ya Gadi! Gadi huishi huko kama simba, akirarua kwenye mkono au kichwa.
21
Alijichagulia nchi nzuri kuliko zote kwa ajili yake mwenyewe; fungu la kiongozi lilikuwa limehifadhiwa kwa ajili yake. Viongozi wa watu walipokusanyika, alitimiza haki ya mapenzi ya Bwana, na hukumu zake kuhusu Israeli.”
22
Kuhusu Dani akasema: “Dani ni mwana simba, akiruka kutoka Bashani.”
23
Kuhusu Naftali akasema: “Naftali amejaa tele upendeleo wa Bwana, naye amejaa baraka yake; atarithi magharibi na kusini.”
24
Kuhusu Asheri akasema: “Aliyebarikiwa zaidi sana katika wana ni Asheri; yeye na apate upendeleo kwa ndugu zake, yeye na anawe miguu yake kwenye mafuta.
25
Makomeo ya malango yako yawe chuma na shaba, nazo nguvu zako zitakuwa sawa na siku zako.
26
“Hakuna mwingine kama Mungu wa Yeshuruni, ambaye hupanda juu ya mbingu ili akusaidie, na juu ya mawingu katika utukufu wake.
27
Mungu wa milele ni kimbilio lako, na chini kuna mikono ya milele. Atamfukuza adui yako mbele yako, akisema, ‘Mwangamize yeye!’
28
Hivyo Israeli ataishi salama peke yake. Mzao wa Yakobo ni salama katika nchi ya nafaka na divai mpya, mahali ambapo mbingu hudondosha umande.
29
Ee Israeli, wewe umebarikiwa! Ni nani kama wewe, taifa lililookolewa na Bwana? Yeye ni ngao yako na msaada wako, na upanga wako uliotukuka. Adui zako watatetemeka mbele yako, nawe utapakanyaga mahali pao pa juu.”
Settings