Matendo 15:7-21
7
Baada ya majadiliano mengi, Petro akasimama na kusema, “Ndugu zangu, mnajua kwamba siku za kwanza Mungu alinichagua ili kwa midomo yangu watu wa Mataifa wapate kusikia ujumbe wa Injili na kuamini.
8
Mungu, yeye ajuaye mioyo, alionyesha kwamba anawakubali kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama vile alivyotupa sisi.
9
Mungu hakutofautisha kati yetu na wao, bali alitakasa mioyo yao kwa imani.
10
Sasa basi, mbona mnataka kumjaribu Mungu kwa kuweka kongwa shingoni mwa wanafunzi ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulibeba?
11
Lakini sisi tunaamini ya kuwa tunaokolewa kwa neema ya Bwana Yesu Kristo, kama wao wanavyookolewa.”
12
Kusanyiko lote likakaa kimya, wakawasikiliza Paulo na Barnaba wakieleza jinsi Mungu alivyowatumia kutenda ishara na maajabu kwa watu wa Mataifa.
13
Walipomaliza kunena, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni.
14
Simoni amekwisha kutueleza jinsi Mungu, kwa mara ya kwanza alivyoonyesha kuhusika kwa kujichagulia watu kutoka watu wa Mataifa kwa ajili ya Jina lake.
15
Maneno ya manabii yanakubaliana na jambo hili, kama ilivyoandikwa:
16
“ ‘Baada ya mambo haya nitarudi, nami nitajenga upya nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena magofu yake na kuisimamisha,
17
ili wanadamu wengine wote wapate kumtafuta Bwana, hata wale watu wa Mataifa wote ambao wanaitwa kwa Jina langu, asema Bwana, afanyaye mambo haya’
18
ambayo yamejulikana tangu zamani.
19
“Kwa hivyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwataabishe watu wa Mataifa wanaomgeukia Mungu.
20
Badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe na vyakula vilivyonajisiwa kwa kutolewa sanamu, wajiepushe na uasherati, au kula mnyama aliyenyongwa, na damu.
21
Kwa maana katika kila mji kwa vizazi vilivyopita, Mose amekuwa na wale wanaotangaza sheria yake kwa kuwa imekuwa ikisomwa kwa sauti kubwa katika masinagogi kila Sabato.”
Settings