2 Samweli 12:15-23
15
Baada ya Nathani kurudi nyumbani kwake, Bwana akampiga yule mtoto ambaye mke wa Uria alikuwa amemzalia Daudi, akaugua.
16
Daudi akamwomba Mungu kwa ajili ya mtoto. Akafunga na akaingia ndani ya nyumba yake akawa siku zote analala sakafuni usiku kucha.
17
Wazee wa nyumbani mwake wakamwendea wakasimama karibu naye ili kumwamsha kutoka pale sakafuni, lakini akakataa, wala hakula chochote pamoja nao.
18
Kunako siku ya saba yule mtoto akafa. Watumishi wa Daudi wakaogopa kumwambia kuwa mtoto amekufa, kwa maana walifikiri, “Wakati mtoto alipokuwa angali hai, tulizungumza na Daudi lakini hakutusikiliza. Tutawezaje kumwambia kwamba mtoto amekufa? Anaweza kufanya kitu cha kujidhuru.”
19
Daudi akaona kuwa watumishi wake wananongʼonezana wenyewe, naye akatambua kuwa mtoto alikuwa amekufa. Akauliza “Je, ni kwamba huyo mtoto amekufa?” Wakamjibu, “Ndiyo, mtoto amekufa.”
20
Basi Daudi akainuka kutoka pale sakafuni. Baada ya kuoga, akajipaka mafuta na kubadilisha nguo zake kisha akaenda ndani ya nyumba ya Bwana, akaabudu. Baada ya hapo akaenda nyumbani kwake kwa kutaka kwake, wakamwandalia chakula, naye akala.
21
Watumishi wake wakamuuliza, “Kwa nini unafanya hivi? Mtoto alipokuwa angali hai, ulifunga na kulia; lakini sasa mtoto amekufa, umeinuka na kula.”
22
Akajibu, “Wakati mtoto alipokuwa bado yungali hai, nilifunga na kulia. Nilifikiri, ‘Nani ajuaye? Bwana aweza kunirehemu ili kumwacha mtoto aishi.’
23
Lakini sasa kwa kuwa amekufa, kwa nini nifunge? Je, naweza kumrudisha tena? Mimi nitakwenda kwake, lakini yeye hatanirudia mimi.”
Settings