2 Wafalme 9:24-37
24
Kisha Yehu akatwaa upinde wake na kumchoma Yoramu katikati ya mabega. Mshale ukapenya kwenye moyo wake, naye akaanguka ghafula ndani ya gari lake.
25
Yehu akamwambia Bidkari, mwendeshaji wa gari lake, “Mwinue na umtupe katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. Kumbuka jinsi mimi na wewe tulivyokuwa tukiendesha pamoja magari yetu nyuma ya Ahabu baba yake, wakati Bwana alipotoa unabii huu kumhusu:
26
‘Jana niliona damu ya Nabothi na damu ya wanawe, nami kwa hakika nitakufanya uilipe juu ya shamba hili, asema Bwana.’ Sasa basi, mwinue na umtupe juu ya kiwanja, kulingana na neno la Bwana.”
27
Wakati Ahazia mfalme wa Yuda alipoona kilichotokea, akakimbia kupitia barabara ya Beth-Hagani. Yehu akamkimbiza akipaza sauti na kusema, “Muue naye pia!” Wakamjeruhi katika gari lake kwenye njia ielekeayo Guri karibu na Ibleamu, lakini akatorokea Megido na akafia huko.
28
Watumishi wake wakambeba kwa gari la vita na kumpeleka Yerusalemu, wakamzika pamoja na baba zake kwenye kaburi lake katika Mji wa Daudi.
29
(Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala katika Yuda.)
30
Kisha Yehu akaenda Yezreeli. Yezebeli aliposikia habari hii, akayapaka macho yake rangi, akatengeneza nywele zake na kutazama nje dirishani.
31
Yehu alipokuwa akiingia langoni, Yezebeli akasema, “Je, umekuja kwa amani, Zimri, wewe muuaji wa bwana wako?”
32
Yehu akaangalia juu dirishani na kuita, “Je, ni nani aliye upande wangu? Ni nani?” Matowashi wawili au watatu wakamtazama.
33
Yehu akasema, “Mtupeni huyo mwanamke chini!” Kwa hiyo wakamtupa chini, nayo baadhi ya damu yake ikatapanyika ukutani na nyingine juu ya farasi walipokuwa wakimkanyaga kwa miguu yao.
34
Yehu akaingia ndani, akala na akanywa. Akasema, “Mshughulikieni huyo mwanamke aliyelaaniwa. Mzikeni, kwa sababu alikuwa binti wa mfalme.”
35
Lakini walipotoka kwenda kumzika, hawakukuta kitu chochote isipokuwa fuvu la kichwa, miguu yake na mikono.
36
Wakarudi na kumwambia Yehu, ambaye alisema, “Hili ndilo neno la Bwana alilosema kupitia kinywa cha mtumishi wake Eliya Mtishbi, kwamba: Katika kiwanja cha Yezreeli, mbwa wataikula nyama ya Yezebeli.
37
Maiti ya Yezebeli itakuwa kama mavi shambani katika uwanja wa Yezreeli, kwamba hakutakuwepo mtu atakayeweza kusema, ‘Huyu ndiye Yezebeli.’ ”
Settings