Skip to content
2 Wafalme 19:20-34

2 Wafalme 19:20-34

20
Kisha Isaya mwana wa Amozi akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akasema: “Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: Nimesikia maombi yako kuhusu Senakeribu mfalme wa Ashuru.
21
Hili ndilo neno ambalo Bwana amelisema dhidi yake: “ ‘Bikira Binti Sayuni anakudharau na kukudhihaki. Binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake unapokimbia.
22
Ni nani uliyemtukana na kumkufuru? Ni nani uliyeinua sauti yako dhidi yake, na kumwinulia macho yako kwa kiburi? Ni dhidi ya yule Aliye Mtakatifu wa Israeli!
23
Kupitia kwa wajumbe wako umelundika matukano juu ya Bwana. Nawe umesema, “Kwa magari yangu mengi ya vita, nimepanda juu ya vilele vya milima, vilele vya juu sana katika Lebanoni. Nami nimeiangusha mierezi yake mirefu, misunobari yake iliyo bora sana. Nimefikia sehemu zake zilizo mbali sana, misitu yake iliyo mizuri sana.
24
Nimechimba visima katika nchi za kigeni na kunywa maji yake. Kwa nyayo za miguu yangu nimekausha vijito vyote vya Misri.”
25
“ ‘Je, hujasikia? Zamani sana niliamuru hili. Siku za kale nilipanga hili; sasa nimelifanya litokee, kwamba umegeuza miji yenye ngome kuwa malundo ya mawe.
26
Watu wa miji hiyo wameishiwa nguvu, wanavunjika mioyo na kuaibishwa. Wao ni kama mimea katika shamba, kama machipukizi mororo ya kijani, kama majani yachipuayo juu ya paa la nyumba, ambayo hukauka kabla ya kukua.
27
“ ‘Lakini ninajua mahali ukaapo, kutoka kwako na kuingia kwako, na jinsi unavyoghadhibika dhidi yangu.
28
Kwa sababu unaghadhibika dhidi yangu, na ufidhuli wako umefika masikioni mwangu, nitaweka ndoana yangu puani mwako na hatamu yangu kinywani mwako, nami nitakufanya urudi kwa njia ile uliyoijia.’
29
“Hii ndiyo itakuwa ishara kwako, ee Hezekia: “Mwaka huu utakula kile kiotacho chenyewe, na mwaka wa pili utakula kutoka machipukizi yake. Lakini katika mwaka wa tatu, panda na uvune, panda mashamba ya mizabibu na ule matunda yake.
30
Mara nyingine tena mabaki ya nyumba ya Yuda wataeneza mizizi chini na kuzaa matunda juu.
31
Kwa kuwa kutoka Yerusalemu watakuja mabaki, na kutoka Mlima Sayuni kundi la walionusurika. Wivu wa Bwana Mwenye Nguvu Zote ndio utatimiza jambo hili.
32
“Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana kuhusu mfalme wa Ashuru: “Hataingia katika mji huu wala hatapiga mshale hapa. Hatakuja mbele yake akiwa na ngao, wala kupanga majeshi kuuzingira.
33
Kwa njia ile aliyoijia, ndiyo atakayorudi; hataingia katika mji huu, asema Bwana.
34
Nitaulinda mji huu na kuuokoa, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu.”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options