2 Wafalme 17:7-18
7
Yote haya yalitokea kwa sababu Waisraeli walikuwa wametenda dhambi dhidi ya Bwana Mungu wao, ambaye alikuwa amewapandisha kutoka Misri akiwatoa chini ya utawala wa nguvu wa Farao mfalme wa Misri. Waliabudu miungu mingine
8
na kufuata desturi za mataifa ambayo Bwana alikuwa ameyafukuza mbele yao, pamoja na desturi ambazo wafalme wa Israeli walizileta.
9
Waisraeli wakafanya vitu kwa siri dhidi ya Bwana Mungu wao, ambavyo havikuwa sawa. Kuanzia kwenye mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye maboma walijijengea wenyewe mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji yao yote.
10
Wakaweka mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda.
11
Wakafukiza uvumba kila mahali palipoinuka, kama yalivyofanya yale mataifa ambayo Bwana alikuwa ameyafukuza mbele yao. Wakafanya mambo maovu ambayo yalimghadhibisha Bwana.
12
Wakaabudu sanamu, ingawa Bwana alikuwa amesema, “Msifanye mambo haya.”
13
Bwana akawaonya Israeli na Yuda kupitia kwa manabii na waonaji wake wote: “Acheni njia zenu mbaya. Shikeni amri na maagizo yangu, kufuatana na sheria yangu yote niliyowaagiza baba zenu kuitii ambayo niliileta kwenu kupitia kwa watumishi wangu manabii.”
14
Lakini hawakusikiliza, walikuwa na shingo ngumu kama baba zao, ambao hawakumtegemea Bwana Mungu wao.
15
Walizikataa amri zake, na agano alilokuwa amelifanya na baba zao, na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu zisizofaa, nao wenyewe wakawa hawafai. Wakayaiga mataifa yaliyowazunguka, ingawa Bwana alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya,” nao wakafanya mambo ambayo Bwana alikuwa amewakataza wasifanye.
16
Wakayaacha maagizo yote ya Bwana Mungu wao na kujitengenezea sanamu mbili, walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, na wakamtumikia Baali.
17
Wakawatoa kafara wana wao na mabinti zao katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa Bwana, wakamghadhibisha.
18
Basi Bwana akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu lililobaki;
Settings