2 Nyakati 31:2-11
2
Hezekia akawapanga makuhani na Walawi katika migawanyo, kila mgawanyo kulingana na wajibu wao, kama ni makuhani au Walawi, ili kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, kuhudumu, kushukuru na kuimba sifa katika malango ya makao ya Bwana.
3
Mfalme akatoa matoleo kutoka mali zake mwenyewe kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na za jioni na sadaka za kuteketezwa kwa siku za Sabato, kwa Sikukuu za Mwezi Mwandamo na kwa ajili ya sikukuu zilizoamriwa kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Bwana.
4
Akawaagiza watu wanaoishi Yerusalemu watoe sehemu iliyo haki ya makuhani na Walawi ili waweze kujitoa kikamilifu kutimiza wajibu wao katika Sheria ya Bwana.
5
Mara tu baada ya kutolewa tangazo hilo, Waisraeli wakatoa kwa ukarimu malimbuko ya nafaka zao, divai mpya, mafuta na asali pamoja na vyote vilivyotoka mashambani. Wakaleta kiasi kikubwa cha fungu la kumi la kila kitu.
6
Watu wa Israeli na Yuda walioishi katika miji ya Yuda wakaleta pia fungu la kumi la makundi yao ya ngʼombe na makundi ya kondoo na mbuzi pia na fungu la kumi la vitu vitakatifu vilivyowekwa wakfu kwa ajili ya Bwana Mungu wao na kuvikusanya katika malundo.
7
Wakaanza kufanya haya katika mwezi wa tatu na kumaliza katika mwezi wa saba.
8
Wakati Hezekia na maafisa wake walipokuja na kuona yale malundo, wakamsifu Bwana na kuwabariki watu wake Israeli.
9
Hezekia akawauliza makuhani na Walawi kuhusu yale malundo,
10
naye Azaria aliyekuwa kuhani mkuu, kutoka jamaa ya Sadoki, akajibu, “Tangu watu walipoanza kuleta sadaka zao katika Hekalu la Bwana tumekuwa na chakula cha kutosha na vingi vya kuweka akiba kwa sababu Bwana amewabariki watu wake, hivyo tumekuwa na kiasi kingi kilichobaki.”
11
Hezekia akatoa agizo la kutengeneza vyumba vya ghala katika Hekalu la Bwana nalo hili likafanyika.
Settings