2 Nyakati 22:1-9
1
Watu wa Yerusalemu wakamfanya Ahazia, mdogo wa wote wa wana wa Yerohamu, kuwa mfalme mahali pa baba yake, kwa sababu washambuliaji wa ghafula waliokuwa wameingia kambini pamoja na Waarabu, walikuwa wamewaua wana wakubwa wote wa Yehoramu. Kwa hiyo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akaanza kutawala.
2
Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia, mjukuu wa Omri.
3
Ahazia naye akaenenda katika njia za nyumba ya Ahabu, kwa sababu mama yake alimshawishi katika kutenda maovu.
4
Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana kama walivyokuwa wamefanya nyumba ya Ahabu, kwa kuwa baada ya kufa kwa baba yake nyumba ya Ahabu ndio waliokuwa washauri wake, kwa uangamivu wake.
5
Pia akafuata shauri lao alipokwenda pamoja na Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu.
6
Hivyo akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyojeruhiwa huko Ramothi alipopigana na Hazaeli mfalme wa Aramu. Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu, mfalme wa Yuda, akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu, kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.
7
Mungu alikuwa ameamuru kwamba kuanguka kwa Ahazia kungetokea atakapokwenda kumwona Yoramu. Ahazia alipowasili, wakatoka pamoja na Yoramu ili kwenda kukutana na Yehu mwana wa Nimshi, ambaye Bwana alikuwa amemtia mafuta kuangamiza nyumba ya Ahabu.
8
Yehu alipokuwa anatekeleza hukumu juu ya nyumba ya Ahabu, akawakuta wakuu wa Yuda na wana wa jamaa ya Ahazia waliokuwa wanamhudumia Ahazia, naye akawaua.
9
Ndipo akaenda kumsaka Ahazia, nao watu wake wakamkamata alipokuwa amejificha huko Samaria. Akaletwa kwa Yehu, naye Yehu akamuua. Wakamzika kwani walisema, “Alikuwa mwana wa Yehoshafati, ambaye alimtafuta Bwana kwa moyo wake wote.” Hivyo hapakuwa na mtu mwenye uwezo katika nyumba ya Ahazia aliyeweza kushika ufalme.
Settings