Wimbo 7:1-9
1
Ee binti wa mwana wa mfalme, tazama jinsi inavyopendeza miguu yako katika viatu! Miguu yako yenye madaha ni kama vito vya thamani, kazi ya mikono ya fundi stadi.
2
Kitovu chako ni kama bilauri ya mviringo ambayo kamwe haikosi divai iliyochanganywa. Kiuno chako ni kichuguu cha ngano kilichozungukwa kwa yungiyungi.
3
Matiti yako ni kama wana-paa wawili, mapacha wa paa.
4
Shingo yako ni kama mnara wa pembe ya ndovu. Macho yako ni vidimbwi vya Heshboni karibu na lango la Beth-Rabi. Pua lako ni kama mnara wa Lebanoni ukitazama kuelekea Dameski.
5
Kichwa chako kinakuvika taji kama mlima Karmeli. Nywele zako ni kama zulia la urujuani; mfalme ametekwa na mashungi yake.
6
Tazama jinsi ulivyo mzuri na unavyopendeza, ee pendo, kwa uzuri wako!
7
Umbo lako ni kama la mtende, nayo matiti yako kama vishada vya matunda.
8
Nilisema, “Nitakwea mtende, nami nitayashika matunda yake.” Matiti yako na yawe kama vishada vya mzabibu, harufu nzuri ya pumzi yako kama matofaa,
9
na kinywa chako kama divai bora kuliko zote. Mpendwa Divai na iende moja kwa moja hadi kwa mpenzi wangu, ikitiririka polepole juu ya midomo na meno.
Settings