Warumi 11:22-36
22
Angalia basi wema na ukali wa Mungu: Kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, kama utadumu katika wema wake. La sivyo, nawe utakatiliwa mbali.
23
Wao nao wasipodumu katika kutokuamini kwao, watapandikizwa tena kwenye shina, kwa maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena kwenye hilo shina.
24
Ikiwa wewe ulikatwa kutoka kile ambacho kwa asili ni mzeituni mwitu na kupandikizwa kinyume cha asili kwenye mzeituni uliopandwa, si rahisi zaidi matawi haya ya asili kupandikizwa tena kwenye shina lake la mzeituni!
25
Ndugu zangu, ili msije mkajidai kuwa wenye hekima kuliko mlivyo, nataka mfahamu siri hii: Ugumu umewapata Israeli kwa sehemu hadi idadi ya watu wa Mataifa watakaoingia itimie.
26
Hivyo Israeli wote wataokolewa. Kama ilivyoandikwa: “Mkombozi atakuja kutoka Sayuni; ataondoa kutokumcha Mungu katika Yakobo.
27
Hili ndilo agano langu nao nitakapoziondoa dhambi zao.”
28
Kwa habari ya Injili, wao ni adui wa Mungu kwa ajili yenu, lakini kuhusu kule kuteuliwa kwao ni wapendwa, kwa ajili ya mababa zao wa zamani,
29
kwa maana akishawapa watu karama, Mungu haziondoi, wala wito wake.
30
Kama vile ninyi wakati fulani mlivyokuwa waasi kwa Mungu lakini sasa mmepata rehema kwa sababu ya kutokutii kwao,
31
hivyo nao Waisraeli wamekuwa waasi ili kwamba wao nao sasa waweze kupata rehema kwa ajili ya rehema za Mungu kwenu.
32
Kwa maana Mungu amewafunga wanadamu wote kwenye kuasi ili apate kuwarehemu wote.
33
Tazama jinsi kilivyo kina cha utajiri wa hekima na maarifa ya Mungu! Tazama jinsi ambavyo hukumu zake hazichunguziki, na ambavyo njia zake zisivyotafutikana!
34
“Ni nani aliyeyafahamu mawazo ya Bwana? Au ni nani ambaye amekuwa mshauri wake?”
35
“Au ni nani aliyempa chochote ili arudishiwe?”
36
Kwa maana vitu vyote vyatoka kwake, viko kwake na kwa ajili yake. Utukufu ni wake milele! Amen.
Settings