Skip to content
Walawi 13:1-28

Walawi 13:1-28

1
Bwana akawaambia Mose na Aroni,
2
“Iwapo mtu yeyote atakuwa na uvimbe au upele au alama nyeupe juu ya ngozi yake ambayo yaweza kuwa ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa Aroni kuhani ama kwa wanawe, kuhani mmojawapo.
3
Kuhani atachunguza hicho kidonda kilichopo juu ya ngozi yake, na kama nywele za mahali palipo na kidonda zimebadilika kuwa nyeupe, na ikiwa kidonda kimeingia ndani ya ngozi, basi ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma. Kuhani atakapomchunguza, atamtangaza mtu huyo kuwa ni najisi kwa kawaida ya ibada.
4
Kama alama juu ya ngozi yake ni nyeupe, lakini haionekani kuwa imeingia ndani zaidi ya ngozi, na nywele kwenye alama hiyo hazijageuka kuwa nyeupe, kuhani atamtenga mtu huyo mahali pa pekee kwa siku saba.
5
Siku ya saba, kuhani atamchunguza, na kama hakuona badiliko kwenye kile kidonda na hakijaenea juu ya ngozi, atamtenga kwa siku nyingine saba.
6
Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama kidonda kimepungua na hakijaenea juu ya ngozi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa ni safi, ni upele tu. Ni lazima mtu huyo afue mavazi yake, naye atakuwa safi.
7
Lakini ikiwa ule upele utaenea juu ya ngozi yake baada ya yeye kujionyesha kwa kuhani na kutangazwa kuwa safi, ni lazima aende tena kwa kuhani.
8
Kuhani atamchunguza, na kama upele umeenea kwenye ngozi, atamtangaza kuwa najisi, kwani ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma.
9
“Wakati mtu yeyote ana ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa kuhani.
10
Kuhani atamchunguza na kama kuna uvimbe mweupe juu ya ngozi ambao umefanya nywele kuwa nyeupe, na kama kuna nyama mbichi ndani ya uvimbe,
11
ni ugonjwa sugu wa ngozi, na kuhani atamtangaza kuwa najisi. Hatamtenga tena kwa sababu ni najisi tayari.
12
“Ikiwa ugonjwa utakuwa umeenea kwenye ngozi yake yote kwa kadiri kuhani atakavyoweza kuona, kwamba umeenea kwenye ngozi yote ya huyo mgonjwa kutoka kichwani mpaka wayo,
13
kuhani atamchunguza, na kama ugonjwa umeenea mwili mzima, atamtangaza huyo mtu kuwa safi. Kwa kuwa mwili wote umekuwa mweupe, yeye ni safi.
14
Lakini itokeapo nyama mbichi kwenye ngozi yake, atakuwa najisi.
15
Kuhani atakapoiona hiyo nyama mbichi, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hiyo nyama mbichi ni najisi, ana ugonjwa wa kuambukiza.
16
Hiyo nyama mbichi ikigeuka na kuwa nyeupe, ni lazima amwendee kuhani.
17
Kuhani atamchunguza, na kama vidonda vimekuwa vyeupe, kuhani atamtangaza mgonjwa huyo kuwa safi; kisha atakuwa safi.
18
“Wakati mtu ana jipu juu ya ngozi yake nalo likapona,
19
napo mahali palipokuwa na jipu pakatokea uvimbe mweupe, au alama yenye wekundu na weupe, ni lazima akajionyeshe kwa kuhani.
20
Kuhani atapachunguza, na kama uvimbe umezama ndani ya ngozi, na nywele zimegeuka kuwa nyeupe, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza uliojitokeza pale jipu lilipokuwa.
21
Lakini ikiwa wakati kuhani anapopachunguza pakawa hapana nywele nyeupe ndani yake, wala hakuna shimo bali pamepungua, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku saba.
22
Kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
23
Lakini ikiwa ile alama haijabadilika wala kuenea, ni kovu tu kutokana na jipu, kuhani atamtangaza kuwa safi.
24
“Wakati mtu ameungua kwenye ngozi yake, pakatokea alama yenye wekundu na weupe, au alama nyeupe ikaonekana penye nyama mbichi pale palipoungua,
25
kuhani ataichunguza ile alama, na kama nywele zilizoko juu yake zimegeuka kuwa nyeupe, napo pametokea shimo, basi huo ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza ambao umetokea juu ya jeraha la moto. Kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
26
Lakini kama kuhani akichunguza na kuona kwamba hakuna nywele nyeupe kwenye alama ile, wala hakuna shimo napo pameanza kupungua, basi kuhani atamtenga kwa siku saba.
27
Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza.
28
Lakini, kama alama ile haikubadilika na wala haijaenea kwenye ngozi, napo pamepungua, ni uvimbe kutokana na jeraha la moto, na kuhani atamtangaza kuwa safi; ni kovu tu kutokana na kuungua.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options