Maombolezo 3:7-31
7
Amenizungushia ukuta ili nisiweze kutoroka, amenifunga kwa minyororo mizito.
8
Hata ninapoita au kulia ili kuomba msaada, anakataa kupokea maombi yangu.
9
Ameizuia njia yangu kwa mapande ya mawe, amepotosha njia zangu.
10
Kama dubu aviziaye, kama simba mafichoni,
11
ameniburuta kutoka njia, akanirarua na kuniacha bila msaada.
12
Amevuta upinde wake na kunifanya mimi niwe lengo kwa ajili ya mishale yake.
13
Alinichoma moyo wangu kwa mishale iliyotoka kwenye podo lake.
14
Nimekuwa kichekesho kwa watu wangu wote, wananidhihaki kwa wimbo mchana kutwa.
15
Amenijaza kwa majani machungu na kunishibisha kwa nyongo.
16
Amevunja meno yangu kwa changarawe, amenikanyagia mavumbini.
17
Amani yangu imeondolewa, nimesahau kufanikiwa ni nini.
18
Kwa hiyo nasema, “Fahari yangu imeondoka na yale yote niliyokuwa nimetarajia kutoka kwa Bwana.”
19
Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu, uchungu na nyongo.
20
Ninayakumbuka vyema, nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu.
21
Hata hivyo najikumbusha neno hili na kwa hiyo ninalo tumaini.
22
Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii, kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe.
23
Ni mpya kila asubuhi, uaminifu wako ni mkuu.
24
Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu, kwa hiyo nitamngojea.”
25
Bwana ni mwema kwa wale ambao tumaini lao ni kwake, kwa yule ambaye humtafuta;
26
ni vyema kungojea kwa utulivu kwa ajili ya wokovu wa Bwana.
27
Ni vyema mtu kuchukua nira bado angali kijana.
28
Na akae peke yake awe kimya, kwa maana Bwana ameiweka juu yake.
29
Na azike uso wake mavumbini bado panawezekana kuwa na matumaini.
30
Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye, na ajazwe na aibu.
31
Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali na Bwana milele.
Settings