Skip to content
Yeremia 4:19-31

Yeremia 4:19-31

19
Ee mtima wangu, mtima wangu! Ninagaagaa kwa maumivu. Ee maumivu makuu ya moyo wangu! Moyo wangu umefadhaika ndani yangu, siwezi kunyamaza. Kwa sababu nimesikia sauti ya tarumbeta, nimesikia kelele ya vita.
20
Maafa baada ya maafa, nchi yote imekuwa magofu. Kwa ghafula mahema yangu yameangamizwa, makazi yangu kwa muda mfupi.
21
Hata lini nitaendelea kuona bendera ya vita na kusikia sauti za tarumbeta?
22
“Watu wangu ni wapumbavu, hawanijui mimi. Ni watoto wasio na akili, hawana ufahamu. Ni hodari kutenda mabaya, hawajui kutenda yaliyo mema.”
23
Niliitazama dunia, nayo haikuwa na umbo tena ni tupu; niliziangalia mbingu, mianga ilikuwa imetoweka.
24
Niliitazama milima, nayo ilikuwa ikitetemeka, vilima vyote vilikuwa vikiyumbayumba.
25
Nilitazama, wala watu hawakuwepo; kila ndege wa angani alikuwa ameruka zake.
26
Nilitazama, hata nchi iliyokuwa imestawi vizuri imekuwa jangwa, miji yake yote ilikuwa magofu mbele za Bwana, mbele ya hasira yake kali.
27
Hivi ndivyo Bwana asemavyo: “Nchi yote itaharibiwa, ingawa sitaiangamiza kabisa.
28
Kwa hiyo dunia itaomboleza na mbingu zilizo juu zitakuwa giza, kwa sababu nimesema nami sitarudi nyuma, nimeamua na wala sitageuka.”
29
Kwa sauti ya wapanda farasi na wapiga upinde kila mji unakimbia. Baadhi wanakimbilia vichakani, baadhi wanapanda juu ya miamba. Miji yote imeachwa, hakuna aishiye ndani yake.
30
Unafanya nini, ewe uliyeharibiwa? Kwa nini unajivika vazi jekundu na kuvaa vito vya dhahabu? Kwa nini unapaka macho yako rangi? Unajipamba bure. Wapenzi wako wanakudharau, wanautafuta uhai wako.
31
Nasikia kilio kama cha mwanamke katika utungu wa kuzaa, kilio cha uchungu kama cha anayemzaa mtoto wake wa kwanza: kilio cha Binti Sayuni akitweta ili aweze kupumua, akiinua mikono yake, akisema, “Ole wangu! Ninazimia; maisha yangu yamekabidhiwa kwa wauaji.”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options