Yeremia 38:14-28
14
Ndipo Mfalme Sedekia akatuma watu wamwitie nabii Yeremia wamlete kwake kwenye ingilio la tatu la Hekalu la Bwana. Mfalme akamwambia Yeremia, “Ninataka kukuuliza jambo fulani, usinifiche kitu chochote.”
15
Yeremia akamwambia Sedekia, “Nikikupa jibu, je, hutaniua? Hata kama nikikupa shauri, wewe hutanisikiliza.”
16
Lakini Mfalme Sedekia akamwapia Yeremia kiapo hiki kwa siri, akisema, “Hakika kama aishivyo Bwana, ambaye ametupa pumzi, sitakuua wala sitakutia mikononi mwa wale wanaotafuta uhai wako.”
17
Kisha Yeremia akamwambia Sedekia, “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: ‘Ikiwa utajisalimisha kwa maafisa wa mfalme wa Babeli, maisha yako yatasalimika, na mji huu hautateketezwa kwa moto. Pia wewe na jamaa yako mtaishi.
18
Lakini ikiwa hutajisalimisha kwa maafisa wa mfalme wa Babeli, mji huu utatiwa mikononi mwa Wakaldayo na watauteketeza kwa moto, nawe mwenyewe hutaweza kujiokoa mikononi mwao.’ ”
19
Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, “Ninawaogopa Wayahudi ambao wamekimbilia kwa Wakaldayo, kwa kuwa Wakaldayo wanaweza kunitia mikononi mwao, nao wakanitenda vibaya.”
20
Yeremia akajibu, “Hawatakutia mikononi mwao. Mtii Bwana kwa kufanya kile ninachokuambia. Kisha utafanikiwa na maisha yako yatakuwa salama.
21
Lakini ukikataa kujisalimisha, hili ndilo Bwana alilonifunulia:
22
Wanawake wote walioachwa katika jumba la kifalme la mfalme wa Yuda wataletwa mbele ya maafisa wa mfalme wa Babeli. Wanawake hao watakuambia: “ ‘Walikupotosha na kukushinda, wale rafiki zako uliowaamini. Miguu yako imezama matopeni; rafiki zako wamekuacha.’
23
“Wake zako wote na watoto wataletwa na kutiwa mikononi mwa Wakaldayo. Wewe mwenyewe hutaweza kujiokoa mikononi mwao. Lakini utatekwa na mfalme wa Babeli, na mji huu utateketezwa kwa moto.”
24
Kisha Sedekia akamwambia Yeremia, “Usiruhusu mtu yeyote ajue kuhusu haya mazungumzo, la sivyo utakufa.
25
Maafisa wakisikia kwamba nimezungumza nawe, nao wakakujia na kusema, ‘Tuambie kile ulichozungumza na mfalme na kile mfalme alichokuambia, usitufiche au sivyo tutakuua,’
26
basi waambie, ‘Nilikuwa ninamsihi mfalme asinirudishe kwenye nyumba ya Yonathani nisije nikafia humo.’ ”
27
Maafisa wote wakamjia Yeremia na kumuuliza, naye Yeremia akawaambia kila kitu mfalme alichomwagiza kusema. Kisha hawakusema lolote zaidi na Yeremia kwa sababu hakuna yeyote aliyesikia mazungumzo yake na mfalme.
28
Naye Yeremia akabaki katika ua wa walinzi hadi siku Yerusalemu ilipotekwa.
Settings