Yeremia 22:20-30
20
“Panda Lebanoni ukapige kelele, sauti yako na isikike huko Bashani, piga kelele toka Abarimu, kwa kuwa wote waliojiunga nawe wameangamizwa.
21
Nilikuonya wakati ulipojisikia kwamba uko salama, lakini ulisema, ‘Mimi sitasikiliza!’ Hii imekuwa kawaida yako tangu ujana wako; hujanitii mimi.
22
Upepo utawaondoa wachungaji wako wote, na wale ulioungana nao wataenda uhamishoni. Kisha utaaibika na kufedheheka kwa sababu ya uovu wako wote.
23
Wewe uishiye Lebanoni, wewe uliyetulia kwenye majengo ya mierezi, tazama jinsi utakavyoomboleza maumivu makali yatakapokupata, maumivu kama yale ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa!
24
“Hakika kama niishivyo,” asema Bwana, “hata kama wewe, Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, ungekuwa pete yangu ya muhuri katika mkono wangu wa kuume, bado ningekungʼoa hapo.
25
Nitakutia mikononi mwa wale wanaotafuta uhai wako, wale unaowaogopa, yaani Nebukadneza mfalme wa Babeli na kwa Wakaldayo.
26
Nitakutupa mbali wewe na mama aliyekuzaa mwende katika nchi nyingine, ambayo hakuna hata mmoja wenu aliyezaliwa huko, nanyi mtafia huko.
27
Kamwe hamtarudi katika nchi mliyotamani kuirudia.”
28
Je, huyu mtu Yekonia ni chungu kilichodharauliwa, chungu kilichovunjika, chombo kisichotakiwa na mtu yeyote? Kwa nini yeye na watoto wake watupwe nje kwa nguvu, na kutupwa kwenye nchi wasioijua?
29
Ee nchi, nchi, nchi, sikia neno la Bwana!
30
Hili ndilo Bwana asemalo: “Mwandike huyu mtu kama asiye na mtoto, mtu ambaye hatafanikiwa maisha yake yote, kwa maana hakuna mtoto wake atakayefanikiwa, wala kukaa kwenye kiti cha enzi cha Daudi wala kuendelea kutawala katika Yuda.”
Settings