Yeremia 15:10-21
10
Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa, mtu ambaye ulimwengu wote unashindana na kugombana naye! Sikukopa wala sikukopesha, lakini kila mmoja ananilaani.
11
Bwana akasema, “Hakika nitakuokoa kwa kusudi jema, hakika nitawafanya adui zako wakuombe msaada nyakati za maafa na nyakati za dhiki.
12
“Je, mtu aweza kuvunja chuma, chuma kitokacho kaskazini, au shaba?
13
Utajiri wako na hazina zako nitavitoa kuwa nyara, bila gharama, kwa sababu ya dhambi zako zote katika nchi yako yote.
14
Nitakufanya uwe mtumwa wa adui zako katika nchi usiyoijua, kwa kuwa katika hasira yangu moto umewashwa utakaowaka juu yako daima.”
15
Wewe unafahamu, Ee Bwana, unikumbuke na unitunze mimi. Lipiza kisasi juu ya watesi wangu. Kwa uvumilivu wako usiniondolee mbali; kumbuka jinsi ninavyoshutumiwa.
16
Maneno yako yalipokuja, niliyala; yakawa shangwe yangu na furaha ya moyo wangu, kwa kuwa nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote.
17
Kamwe sikuketi katika kundi la wafanyao sherehe, wala kamwe sikujifurahisha pamoja nao; niliketi peke yangu kwa sababu mkono wako ulikuwa juu yangu, na wewe ulikuwa umenijaza hasira.
18
Kwa nini maumivu yangu hayakomi, na jeraha langu ni la kuhuzunisha, wala haliponyeki? Je, utakuwa kwangu kama kijito cha udanganyifu, kama chemchemi iliyokauka?
19
Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana: “Kama ukitubu, nitakurejeza ili uweze kunitumikia; kama ukinena maneno yenye maana, wala si ya upuzi, utakuwa mnenaji wangu. Watu hawa ndio watakaokugeukia, wala si wewe utakayewageukia wao.
20
Nitakufanya wewe uwe ukuta kwa watu hawa, ngome ya ukuta wa shaba; watapigana nawe lakini hawatakushinda, kwa maana mimi niko pamoja nawe kukuponya na kukuokoa,” asema Bwana.
21
“Nitakuokoa kutoka mikono ya waovu, na kukukomboa kutoka makucha ya watu wakatili.”
Settings