Skip to content
Yeremia 14:12-22

Yeremia 14:12-22

12
Ingawa wanafunga, sitasikiliza kilio chao; hata wakitoa dhabihu za kuteketezwa na dhabihu za nafaka, sitazikubali. Badala yake, nitawaangamiza kwa upanga, njaa na tauni.”
13
Lakini nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, manabii wanaendelea kuwaambia, ‘Hamtaona upanga wala kukabiliwa na njaa. Naam, nitawapa amani ya kudumu mahali hapa.’ ”
14
Ndipo Bwana akaniambia, “Manabii wanatabiri uongo kwa jina langu. Sikuwatuma, wala sikuwaweka, wala sikusema nao. Wanawatabiria maono ya uongo, maaguzi, maono ya sanamu zisizofaa kitu, na madanganyo ya mawazo yao wenyewe.
15
Kwa hiyo, hili ndilo Bwana asemalo kuhusu manabii wanaotabiri kwa jina langu: Mimi sikuwatuma, lakini wanasema, ‘Hakuna upanga wala njaa itakayoigusa nchi hii.’ Manabii hao hao watakufa kwa upanga na njaa.
16
Nao watu hao wanaowatabiria watatupwa nje katika barabara za Yerusalemu kwa sababu ya njaa na upanga. Hapatakuwepo yeyote wa kuwazika wao au wake zao, wana wao au binti zao. Nitawamwagia maafa wanayostahili.
17
“Nena nao neno hili: “ ‘Macho yangu na yatiririkwe na machozi usiku na mchana bila kukoma; kwa kuwa binti yangu aliye bikira, yaani watu wangu, amepata jeraha baya, pigo la kuangamiza.
18
Kama nikienda mashambani, ninaona wale waliouawa kwa upanga; kama nikienda mjini, ninaona maangamizi ya njaa. Nabii na kuhani kwa pamoja wamekwenda katika nchi wasiyoijua.’ ”
19
Je, umemkataa Yuda kabisa? Umemchukia Sayuni kabisa? Kwa nini umetuumiza hata hatuwezi kuponyeka? Tulitarajia amani, lakini hakuna jema lililotujia; tulitarajia wakati wa kupona lakini kuna hofu kuu tu.
20
Ee Bwana, tunatambua uovu wetu na kosa la baba zetu; kweli tumetenda dhambi dhidi yako.
21
Kwa ajili ya jina lako usituchukie kabisa; usikidharau kiti chako cha enzi kilichotukuka. Kumbuka agano lako nasi na usilivunje.
22
Je, kuna sanamu yoyote isiyofaa kitu ya mataifa iwezayo kuleta mvua? Je, anga peke yake zaweza kutoa mvua? La hasha, ni wewe peke yako, Ee Bwana, Mungu wetu. Kwa hiyo tumaini letu liko kwako, kwa kuwa wewe ndiwe ufanyaye haya yote.
Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options