Isaya 63:11-19
11
Ndipo watu wake wakazikumbuka siku zilizopita, siku za Mose na watu wake: yuko wapi yeye aliyewaleta kupitia katikati ya bahari, pamoja na wachungaji wa kundi lake? Yuko wapi yule aliyeweka Roho wake Mtakatifu katikati yao,
12
aliyetuma mkono wake uliotukuka wenye nguvu kuwa katika mkono wa kuume wa Mose, aliyegawa maji ya bahari mbele yao, ili kujipatia jina milele,
13
aliyewaongoza kupitia kwenye vilindi? Kama farasi katika nchi iliyo wazi, wao hawakujikwaa,
14
kama ngʼombe washukao bondeni kwenye malisho, walipewa pumziko na Roho wa Bwana. Hivi ndivyo ulivyowaongoza watu wako ili kujipatia mwenyewe jina tukufu.
15
Tazama chini kutoka mbinguni ukaone kutoka kiti chako cha enzi kilichoinuliwa juu, kitakatifu na kitukufu. Uko wapi wivu wako na uweza wako? Umetuzuilia wema wako na huruma zako.
16
Lakini wewe ni Baba yetu, ingawa Abrahamu hatufahamu sisi wala Israeli hatutambui; wewe, Ee Bwana, ndiwe Baba yetu, Mkombozi wetu tangu zamani za kale ndilo jina lako.
17
Ee Bwana, kwa nini unatuacha twende mbali na njia zako, na kuifanya mioyo yetu migumu hata hatukukuheshimu? Rudi kwa ajili ya watumishi wako, yale makabila ambayo ni urithi wako.
18
Kwa maana kwa muda mfupi watu wako walimiliki mahali pako patakatifu, lakini sasa adui zetu wamepakanyaga mahali patakatifu pako.
19
Sisi tumekuwa kama wale ambao hujawatawala kamwe, kama wale ambao hawajaitwa kwa jina lako.
Settings