Isaya 10:5-19
5
“Ole kwa Ashuru, fimbo ya hasira yangu, ambaye mkononi mwake ana rungu ya ghadhabu yangu!
6
Ninamtuma dhidi ya taifa lisilomjua Mungu, ninamtuma dhidi ya taifa linalonikasirisha, kukamata mateka na kunyakua nyara, pia kuwakanyaga chini kama matope ya barabarani.
7
Lakini hili silo analokusudia, hili silo alilo nalo akilini; kusudi lake ni kuangamiza, kuyakomesha mataifa mengi.
8
Maana asema, ‘Je, wafalme wote si majemadari wangu?
9
Je, Kalno hakutendwa kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi, nayo Samaria si kama Dameski?
10
Kama vile mkono wangu ulivyotwaa falme za sanamu, falme ambazo vinyago vyao vilizidi vile vya Yerusalemu na Samaria:
11
je, nisiishughulikie Yerusalemu na sanamu zake kama nilivyoshughulikia Samaria na vinyago vyake?’ ”
12
Bwana atakapokuwa amemaliza kazi yake yote dhidi ya Mlima Sayuni na Yerusalemu, atasema, “Nitamwadhibu mfalme wa Ashuru kwa ajili ya majivuno ya ukaidi wa moyo wake na kutazama kwa macho yenye dharau.”
13
Kwa kuwa anasema: “ ‘Kwa nguvu za mkono wangu nimefanya hili, kwa hekima yangu, kwa sababu nina ufahamu. Niliondoa mipaka ya mataifa, niliteka nyara hazina zao, kama yeye aliye shujaa niliwatiisha wafalme wao.
14
Kama mtu atiavyo mkono kwenye kiota, ndivyo mkono wangu ulivyochukua utajiri wa mataifa; kama watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya nchi zote; wala hakuna hata mmoja aliyepiga bawa au kufungua kinywa chake kutoa mlio.’ ”
15
Je, shoka laweza kujigamba kuwa na nguvu zaidi kuliko yule anayelitumia, au msumeno kujisifu dhidi ya yule anayeutumia? Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua yeye aichukuaye, au mkongojo ungemwinua mwenye kuutumia!
16
Kwa hiyo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, atatuma ugonjwa wa kudhoofisha kwa askari wake walio hodari, katika fahari yake moto utawaka kama mwali wa moto.
17
Nuru ya Israeli itakuwa moto, Aliye Mtakatifu wao mwali wa moto; katika siku moja utaunguza na kuteketeza miiba na michongoma yake.
18
Fahari ya misitu yake na mashamba yenye rutuba utateketeza kabisa, kama vile mtu mgonjwa adhoofikavyo.
19
Nayo miti inayobaki katika misitu yake itakuwa michache sana hata mtoto mdogo angeweza kuihesabu.
Settings