Skip to content
Ezekieli 34:11-24

Ezekieli 34:11-24

11
“ ‘Kwa kuwa hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Mimi mwenyewe nitawaulizia kondoo wangu na kuwatafuta.
12
Kama vile mchungaji atafutavyo kundi lake lililotawanyika wakati akiwa pamoja nalo, hivyo ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu. Nitawaokoa kutoka mahali pote walipokuwa wametawanyikia katika siku ya mawingu na giza nene.
13
Nitawatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mbalimbali, nami nitawaleta katika nchi yao wenyewe. Nitawalisha kwenye milima ya Israeli, katika mabonde na mahali pote panapokalika katika nchi.
14
Nitawachunga kwenye malisho mazuri na miinuko ya mlima wa Israeli patakuwa mahali pao pa malisho. Huko watajipumzisha kwa amani katika nchi ya malisho mazuri, nao watajilisha huko katika malisho tele katika milima ya Israeli.
15
Mimi mwenyewe nitawachunga kondoo zangu na kuwafanya wapumzike, asema Bwana Mwenyezi.
16
Nitawaulizia kondoo waliopotea na kuwaleta waliotangatanga. Nitawafunga waliojeruhiwa na kuwatia nguvu walio dhaifu lakini wale waliojikinai na wenye nguvu nitawaangamiza. Nitalichunga kundi kwa haki.
17
“ ‘Kwa habari yenu, enyi kundi langu, hili ndilo Bwana Mwenyezi asemalo: Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo, kati ya kondoo dume na mbuzi.
18
Je, haiwatoshi ninyi kujilisha kwenye malisho mazuri? Je, ni lazima ninyi kuyakanyaga pia malisho yenu yaliyobaki kwa miguu yenu? Je, haiwatoshi ninyi kunywa maji safi? Je, ni lazima kuyachafua maji mengine kwa miguu yenu?
19
Je, ni lazima kundi langu wajilishe kwa yale mliyoyakanyaga na kunywa maji mliyoyachafua kwa miguu yenu?
20
“ ‘Kwa hiyo, hili ndilo Bwana Mwenyezi awaambialo: Tazama, mimi mwenyewe nitahukumu kati ya kondoo wanono na waliokonda.
21
Kwa sababu mmewapiga kikumbo na kuwapiga kwa pembe zenu kondoo wote walio dhaifu mpaka wakawafukuza,
22
nitaliokoa kundi langu na hawatatekwa nyara tena. Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo.
23
Nitaweka juu yao mchungaji mmoja, mtumishi wangu Daudi, naye atawachunga, atawachunga na kuwa mchungaji wao.
24
Mimi Bwana nitakuwa Mungu wao, naye mtumishi wangu Daudi atakuwa mkuu miongoni mwao. Mimi Bwana nimenena.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options