Ezekieli 18:5-18
5
“Mtu aweza kuwa ni mwenye haki atendaye yaliyo haki na sawa.
6
Hakula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima wala hakuziinulia macho sanamu za nyumba ya Israeli. Hakumtia unajisi mke wa jirani yake, wala hakukutana kimwili na mwanamke wakati wa siku zake za hedhi.
7
Hamwonei mtu yeyote, bali hurudisha kilichowekwa rehani kwake. Hanyangʼanyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake na huwapa nguo walio uchi.
8
Hakopeshi kwa riba wala hajipatii faida ya ziada. Huuzuia mkono wake usifanye mabaya, naye huhukumu kwa haki kati ya mtu na mtu.
9
Huzifuata amri zangu na kuzishika sheria zangu kwa uaminifu. Huyo mtu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana Mwenyezi.
10
“Aweza kuwa ana mwana jeuri, amwagaye damu au atendaye mojawapo ya mambo haya
11
(ingawa baba yake hakufanya mojawapo ya haya): “Hula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima. Humtia unajisi mke wa jirani yake.
12
Huwaonea maskini na wahitaji. Hunyangʼanyana. Harudishi kile kilichowekwa rehani kwake. Huziinulia sanamu macho. Hufanya mambo ya machukizo.
13
Hukopesha kwa riba na kutafuta faida ya ziada. Je, mtu wa namna hii ataishi? Hapana, hataishi! Kwa sababu amefanya mambo haya yote ya machukizo, hakika atauawa na damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe.
14
“Lakini yawezekana mwana huyo ana mwana aonaye dhambi hizi zote anazofanya baba yake, naye ingawa anaziona, yeye hafanyi mabaya kama haya:
15
“Hakula katika mahali pa ibada za miungu kwenye milima, wala hainulii macho sanamu za nyumba ya Israeli. Hakumtia unajisi mke wa jirani yake.
16
Hakumwonea mtu yeyote wala hakutaka rehani kwa ajili ya mkopo. Hanyangʼanyi, bali huwapa wenye njaa chakula chake na huwapa nguo walio uchi.
17
Huuzuia mkono wake usitende dhambi, hakopeshi kwa riba wala hajipatii faida ya ziada. Huzishika amri zangu na kuzifuata sheria zangu. Hatakufa kwa ajili ya dhambi za baba yake; hakika ataishi.
18
Lakini baba yake atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe, kwa sababu alitoza bei isiyo halali kwa nguvu, akamnyangʼanya ndugu yake na kufanya yaliyo mabaya miongoni mwa watu wake.
Settings