Kutoka 39:8-21
8
Akafanyiza kifuko cha kifuani, kazi ya fundi stadi. Akakitengeneza kama kile kisibau: cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa.
9
Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri moja na upana wa shibiri moja, nacho kilikunjwa mara mbili.
10
Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za vito vya thamani. Safu ya kwanza ilikuwa na akiki, yakuti manjano na zabarajadi;
11
safu ya pili ilikuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi;
12
safu ya tatu ilikuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto;
13
katika safu ya nne ilikuwa na krisolitho, shohamu na yaspi. Vito hivyo vilitiwa kwenye vijalizo vya dhahabu.
14
Palikuwa na vito kumi na viwili, kila kimoja kikiwa na jina mojawapo la wana wa Israeli; kila kimoja kilichorwa kama muhuri kikiwa na jina mojawapo la yale makabila kumi na mawili.
15
Kwa ajili ya kile kifuko cha kifuani akakitengenezea mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba.
16
Akatengeneza vijalizo viwili vya dhahabu na pete mbili za dhahabu, na kuzifungia pete hizo kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani.
17
Akafunga hiyo mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete katika pembe za hicho kifuko cha kifuani,
18
nazo zile ncha nyingine za mkufu akazifunga kwenye vile vijalizo viwili, na kuzishikamanisha na vile vipande vya mabega vya kile kisibau upande wa mbele.
19
Akatengeneza pete mbili za dhahabu na kuzishikamanisha kwenye pembe mbili za chini, upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kisibau.
20
Kisha akatengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzishikamanisha sehemu ya chini ya vipande vya mabega upande wa mbele wa kile kisibau, karibu na pindo juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kisibau.
21
Akafunga pete za hicho kifuko cha kifuani kwenye pete za kisibau kwa kamba ya buluu, wakiziunganisha na ule mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisisogee kutoka kwenye kile kisibau, kama Bwana alivyomwagiza Mose.
Settings