Danieli 8:3-14
3
Nikatazama juu, na hapo mbele yangu kulikuwa na kondoo dume mwenye pembe mbili, akiwa amesimama kando ya mto, nazo pembe zake zilikuwa ndefu. Pembe moja ilikuwa ndefu kuliko hiyo nyingine, lakini iliendelea kukua baadaye.
4
Nikamtazama yule kondoo dume alivyokuwa akishambulia kuelekea magharibi, kaskazini na kusini. Hakuna mnyama yeyote aliyeweza kusimama dhidi yake, wala hakuna aliyeweza kuokoa kutoka nguvu zake. Alifanya kama atakavyo, naye akawa mkuu.
5
Nilipokuwa ninatafakari hili, ghafula beberu mwenye pembe moja kubwa sana katikati ya macho yake alikuja kutoka magharibi, akiruka kasi juu ya dunia yote bila kugusa ardhi.
6
Alikuja akimwelekea yule kondoo dume mwenye pembe mbili niliyemwona akisimama kando ya mto, akamshambulia kwa hasira nyingi.
7
Nikamwona akimshambulia yule kondoo dume kwa hasira nyingi, akimpiga yule kondoo dume na kuvunja pembe zake mbili. Yule kondoo dume hakuwa na nguvu za kumzuia yule beberu, hivyo akamwangusha yule kondoo dume chini na kumkanyaga, wala hakuna aliyeweza kumwokoa yule kondoo dume kutoka nguvu za huyo beberu.
8
Yule beberu akawa mkubwa sana, lakini katika kilele cha nguvu zake ile pembe yake ndefu ilivunjika, na mahali pake pakaota pembe nne kubwa kuelekea pande nne za dunia.
9
Kutoka mojawapo ya zile pembe nne palitokea pembe ndogo ukaongezeka nguvu kuelekea kusini, na kuelekea mashariki, na kuelekea Nchi ya Kupendeza.
10
Pembe hiyo ikaendelea kukua hadi kufikia jeshi la mbinguni, nayo ikalitupa baadhi ya jeshi la vitu vya angani hapa chini duniani, na kulikanyaga.
11
Pembe hiyo ikajikweza ili iwe kama Mkuu wa hilo jeshi; ikamwondolea dhabihu ya kila siku, napo mahali pake patakatifu pakashushwa chini.
12
Kwa sababu ya uasi, jeshi la watakatifu na dhabihu za kila siku vikatiwa mikononi mwake. Ikafanikiwa katika kila kitu ilichofanya, nayo kweli ikatupwa chini.
13
Kisha nikamsikia mtakatifu mmoja akizungumza na mtakatifu mwingine, akamwambia, “Je, itachukua muda gani maono haya yatimie: maono kuhusu dhabihu ya kila siku, uasi unaosababisha ukiwa, kutwaliwa kwa mahali patakatifu, na jeshi litakalokanyagwa chini ya nyayo?”
14
Akaniambia, “Itachukua siku 2,300. Ndipo mahali patakatifu patawekwa wakfu tena.”
Settings