Danieli 4:10-17
10
Haya ndiyo maono niliyoona nilipokuwa nimelala kitandani mwangu: Nilitazama, na mbele yangu ulisimama mti katikati ya nchi. Ulikuwa mrefu sana.
11
Mti ule ulikua, ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga; ulionekana mpaka miisho ya dunia.
12
Majani yake yalikuwa ya kupendeza, matunda yake yalikuwa mengi, na juu yake kulikuwa na chakula kwa ajili ya wote. Chini ya kivuli chake wanyama wa kondeni walipata hifadhi, na ndege wa angani waliishi katika matawi yake. Kila kiumbe kililishwa kutokana na mti huo.
13
“Katika maono niliyoyaona nikiwa nimelala kitandani mwangu, nilitazama, na mbele yangu alikuwepo mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni.
14
Akaita kwa sauti kubwa: ‘Kateni mti huu, myafyeke matawi yake; yaondoeni majani yake na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na wakimbie kutoka chini yake na ndege waondoke kutoka matawi yake.
15
Lakini acheni kisiki chake na mizizi, kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kibaki ardhini, kwenye majani ya kondeni. “ ‘Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, naye aachwe aishi pamoja na wanyama miongoni mwa mimea ya dunia.
16
Akili yake na ibadilishwe kutoka ile ya mwanadamu na apewe akili ya mnyama, mpaka nyakati saba zipite juu yake.
17
“ ‘Uamuzi huu umetangazwa na walinzi, hukumu imetangazwa na watakatifu, ili walio hai wajue kuwa Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme zote za wanadamu, naye humpa yeyote amtakaye na kumtawaza juu yake hata yeye aliye mnyonge sana miongoni mwa wanadamu.’
Settings