Danieli 2:14-23
14
Wakati Arioko, mkuu wa askari wa walinzi wa mfalme, alikuwa amekwenda kuwaua watu wenye hekima wa Babeli, Danieli akazungumza naye kwa hekima na busara.
15
Akamuuliza huyo afisa wa mfalme, “Kwa nini mfalme ametoa amri kali hivyo?” Ndipo Arioko akamweleza Danieli jambo hilo.
16
Aliposikia jambo hili, Danieli akamwendea mfalme, akamwomba ampe muda ili aweze kumfasiria ile ndoto.
17
Ndipo Danieli akarudi nyumbani kwake na kuwaeleza rafiki zake Hanania, Mishaeli na Azaria jambo hilo.
18
Aliwasihi waombe rehema kutoka kwa Mungu wa mbinguni kuhusu siri hii, ili yeye na rafiki zake wasije wakauawa pamoja na wenye hekima wengine wa Babeli.
19
Wakati wa usiku lile fumbo lilifunuliwa kwa Danieli katika maono. Ndipo Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni,
20
na akasema: “Lihimidiwe jina la Mungu milele na milele; hekima na uweza ni vyake.
21
Yeye hubadili nyakati na majira; huwaweka wafalme na kuwaondoa. Huwapa hekima wenye hekima, na maarifa wenye ufahamu.
22
Hufunua siri na mambo yaliyofichika; anajua yale yaliyo gizani, nayo nuru hukaa kwake.
23
Ninakushukuru na kukuhimidi, Ee Mungu wa baba zangu: Umenipa hekima na uwezo, umenijulisha kile tulichokuomba, umetujulisha ndoto ya mfalme.”
Settings