2 Wafalme 9:13-22
13
Wakaharakisha kuvua mavazi yao, na kuyatandaza chini ya Yehu ili akanyage juu kwenye ngazi ya nje. Kisha wakapiga tarumbeta na kupaza sauti wakisema, “Yehu ni mfalme!”
14
Basi Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akafanya shauri baya dhidi ya Yoramu. (Wakati huu, Yoramu na Israeli wote walikuwa wakiilinda Ramoth-Gileadi dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu,
15
lakini Mfalme Yoramu alikuwa amerudishwa Yezreeli ili kujiuguza kutokana na majeraha ambayo Waaramu walimtia katika vita na Hazaeli mfalme wa Aramu.) Yehu akasema, “Kama hii ndiyo nia yenu, msimruhusu hata mmoja kutoroka nje ya mji kwenda kupeleka habari huko Yezreeli.”
16
Ndipo Yehu akaingia katika gari lake la vita na kuendesha kwenda Yezreeli, kwa sababu Yoramu alikuwa amepumzika huko, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameenda kumwona.
17
Mlinzi aliyesimama juu ya kinara cha Yezreeli alipoona askari wa Yehu wanakuja, akaita akisema, “Naona askari wanakuja.” Yoramu akaamuru, “Mtwae mpanda farasi umtume akakutane nao na kuuliza, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”
18
Mpanda farasi akaondoka kwenda kukutana na Yehu na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme: ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ” Yehu akamjibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.” Mlinzi akatoa habari, “Mjumbe amewafikia lakini harudi.”
19
Basi mfalme akamtuma mpanda farasi wa pili. Wakati alipowafikia akasema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ” Yehu akajibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”
20
Yule mlinzi akatoa taarifa akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini hata yeye harudi. Uendeshaji ule ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi, anaendesha kama mwenye wazimu!”
21
Yoramu akaagiza, akasema, “Weka tayari gari langu la vita.” Na baada ya gari kuwa tayari, Yoramu mfalme wa Israeli, na Ahazia mfalme wa Yuda, wakaondoka kila mmoja kwenye gari lake ili kukutana na Yehu. Walikutana naye katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli.
22
Yoramu alipomwona Yehu akauliza, “Je, Yehu, umekuja kwa amani?” Yehu akajibu, “Kunawezaje kuwa na amani wakati ibada za sanamu na uchawi wa mama yako Yezebeli ungaliko?”
Settings