Skip to content
1 Samweli 6:10-18

1 Samweli 6:10-18

10
Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ngʼombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini.
11
Wakaliweka Sanduku la Bwana juu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu.
12
Kisha hao ngʼombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ngʼombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi.
13
Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona.
14
Lile gari la kukokotwa lilikuja mpaka kwenye shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi, nalo likasimama kando ya mwamba mkubwa. Watu wakapasua mbao za lile gari la kukokotwa na kutoa dhabihu wale ngʼombe kama sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana.
15
Walawi walilishusha Sanduku la Bwana, pamoja na lile kasha lililokuwa na vile vitu vya dhahabu na kuviweka juu ya ule mwamba mkubwa. Siku ile watu wa Beth-Shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu kwa Bwana.
16
Wale watawala watano wa Wafilisti waliona haya yote, nao wakarudi siku ile ile mpaka Ekroni.
17
Haya ndiyo yale majipu ya dhahabu Wafilisti waliyotuma kama sadaka ya hatia kwa Bwana, moja kwa ajili ya Ashdodi, moja kwa Gaza, moja kwa Ashkeloni, moja kwa Gathi, na moja kwa Ekroni.
18
Nayo hesabu ya wale panya wa dhahabu ilikuwa kulingana na idadi ya miji ya Wafilisti ya watawala watano wa Wafilisti: miji yao iliyozungukwa na maboma, pamoja na vijiji vya miji hiyo. Ule mwamba mkubwa, ambao juu yake waliliweka lile Sanduku la Bwana, ni ushahidi hadi leo katika shamba la Yoshua wa Beth-Shemeshi.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options