1 Samweli 6:1-9
1
Sanduku la Bwana lilipokuwa limekaa katika nchi ya Wafilisti kwa miezi saba,
2
Wafilisti waliwaita makuhani wa Dagoni na waaguzi, na kuwaambia, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Bwana? Tuambieni jinsi tutakavyolirudisha mahali pake.”
3
Wakajibu, “Kama mtalirudisha Sanduku la Mungu wa Israeli, msilirudishe mikono mitupu bali kwa vyovyote mpelekeeni sadaka ya hatia. Kisha mtaponywa, nanyi mtafahamu kwa nini mkono wake haujaondolewa kwenu.”
4
Wafilisti wakawauliza, “Ni sadaka gani ya hatia tutakayompelekea?” Wakajibu, “Majipu matano ya dhahabu na panya wa dhahabu watano, kulingana na idadi ya watawala wa Wafilisti, kwa sababu tauni iyo hiyo imewaua ninyi na watawala wenu.
5
Tengenezeni mifano ya majipu na ya panya wale wanaoharibu nchi yenu, nanyi mheshimuni Mungu wa Israeli. Labda ataondoa mkono wake kutoka kwenu na kwa miungu yenu na nchi yenu.
6
Kwa nini ninyi mnafanya mioyo yenu migumu kama Wamisri na Farao walivyofanya? Je, alipowatendea kwa ukali, hawakuwaachia Waisraeli wakaenda zao?
7
“Sasa basi, wekeni gari jipya la kukokotwa pamoja na ngʼombe wawili ambao wamezaa lakini ambao kamwe hawajafungwa nira. Fungieni hao ngʼombe hilo gari, lakini ondoeni ndama wao na mwaweke zizini.
8
Chukueni hilo Sanduku la Bwana na mliweke juu ya gari la kukokotwa, na ndani ya kasha kando yake wekeni hivyo vitu vya dhahabu mnavyompelekea Bwana kama sadaka ya hatia. Lipelekeni,
9
lakini liangalieni kwa makini. Iwapo litakwenda katika nchi yake lenyewe, kuelekea Beth-Shemeshi, basi tutajua kwamba Bwana ndiye alileta haya maafa makubwa juu yetu. Lakini kama halikwenda, basi tutajua kwamba haukuwa mkono wa Bwana uliotupiga na kwamba iliyotokea kwetu ni ajali.”
Settings