Skip to content
1 Wafalme 4:24-34

1 Wafalme 4:24-34

24
Kwa kuwa Solomoni alitawala falme zote magharibi ya mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote.
25
Wakati wa maisha ya Solomoni Yuda na Israeli, kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba, wakaishi salama kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake.
26
Solomoni alikuwa na mabanda 4,000 ya magari ya vita, na farasi 12,000.
27
Maafisa wa eneo hilo, kila mmoja katika mwezi wake, walileta mahitaji kwa ajili ya Mfalme Solomoni na wote waliokula mezani mwa mfalme. Walihakikisha kuwa hakuna chochote kilichopungua.
28
Pia walileta sehemu walizopangiwa za shayiri na majani kwa ajili ya farasi wavutao magari na farasi wengine mahali palipostahili.
29
Mungu akampa Solomoni hekima na akili kubwa, pia ufahamu mpana usiopimika kama mchanga ulioko pwani ya bahari.
30
Hekima ya Solomoni ilikuwa kubwa kuliko hekima ya watu wote wa Mashariki na kubwa kuliko hekima yote ya Misri.
31
Alikuwa na hekima kuliko kila mwandishi, akiwemo Ethani Mwezrahi: kuliko Hemani, Kalkoli na Darda, wana wa Maholi. Umaarufu wake ukaenea kwa mataifa yote yaliyomzunguka.
32
Akanena mithali 3,000 na nyimbo zake zilikuwa 1,005.
33
Akaelezea maisha ya mimea kuanzia mwerezi wa Lebanoni hadi hisopo iotayo ukutani. Pia akafundisha kuhusu wanyama na ndege, wanyama wenye damu baridi, wakiwemo samaki.
34
Watu wa mataifa yote wakaja kusikiliza hekima ya Solomoni, waliotumwa na wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamesikia juu ya hekima yake.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options