Zaburi 98
Ushindi wa Mungu na Wokovu kwa Wote 1–3
1
Zaburi. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; kitanga chake cha kuume na mkono wake mtakatifu umemfanyia wokovu.
2
Bwana ameufanya wokovu wake ujulikane na amedhihirisha haki yake kwa mataifa.
3
Ameukumbuka upendo wake na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli; miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu.
Wito wa Sifa na Ibada kwa Wote 4–6
4
Mpigieni Bwana kelele za shangwe, dunia yote, ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda;
5
mwimbieni Bwana kwa kinubi, kwa kinubi na sauti za kuimba,
6
kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu za pembe za kondoo dume: shangilieni kwa furaha mbele za Bwana, aliye Mfalme.
Uumbaji Wautazamia Hukumu ya Mfalme 7–9
7
Bahari na ivume na kila kiliomo ndani yake, dunia na wote wakaao ndani yake.
8
Mito na ipige makofi, milima na iimbe pamoja kwa furaha,
9
vyote na viimbe mbele za Bwana, kwa maana yuaja kuhukumu dunia. Atahukumu dunia kwa haki na mataifa kwa haki.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Study note