Skip to content

Zaburi 41

Baraka za Kuwahurumia Wanaoteseka 1–3

1
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Heri mtu yule anayemjali mnyonge, Bwana atamwokoa wakati wa shida.
2
Bwana atamlinda na kuyahifadhi maisha yake, atambariki katika nchi na hatamwacha katika tamaa ya adui zake.
3
Bwana atamtegemeza awapo mgonjwa kitandani, atamwinua kutoka kitandani mwake.

Maombolezo na Maombi ya Daudi 4–9

4
Nilisema, “Ee Bwana nihurumie, niponye, maana nimekutenda dhambi wewe.”
5
Adui zangu wanasema kwa hila, “Lini atakufa, na jina lake litokomee kabisa.”
6
Kila anapokuja mtu kunitazama, huzungumza uongo, huku moyo wake hukusanya masingizio; kisha huondoka na kuyasambaza huku na huko.
7
Adui zangu wote hunongʼonezana dhidi yangu, hao huniwazia mabaya sana, wakisema,
8
“Ugonjwa mbaya sana umempata, kamwe hatainuka tena kitandani mwake.”
9
Hata rafiki yangu wa karibu niliyemwamini, yule aliyekula chakula changu ameniinulia kisigino chake.

Ombi la Ujasiri la Wokovu wa Mungu 10–13

10
Lakini wewe, Ee Bwana, nihurumie, ukaniinue tena, ili niweze kuwalipiza kisasi.
11
Najua kwamba wapendezwa nami, kwa kuwa adui yangu hanishindi.
12
Katika uadilifu wangu unanitegemeza na kuniweka kwenye uwepo wako milele.
13
Msifuni Bwana, Mungu wa Israeli, tangu milele na hata milele.

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.