Hesabu 26:52-65
52
Bwana akamwambia Mose,
53
“Watagawiwa nchi kama urithi kwa kulingana na hesabu ya majina.
54
Kundi kubwa zaidi lipe urithi mkubwa zaidi, na kundi dogo zaidi lipewe urithi mdogo zaidi; kila kundi litapokea urithi wake kulingana na hesabu ya wale walioorodheshwa.
55
Hakikisha kuwa nchi inagawanywa kwa kura. Kile kitakachorithiwa na kila kikundi kitakuwa kwa kulingana na majina ya kabila la babu yao.
56
Kila urithi utagawanywa kwa kura miongoni mwa makundi makubwa na madogo.”
57
Hawa walikuwa Walawi ambao walihesabiwa kwa koo zao: kutoka kwa Gershoni, ukoo wa Wagershoni; kutoka kwa Kohathi, ukoo wa Wakohathi; kutoka kwa Merari, ukoo wa Wamerari.
58
Hizi pia zilikuwa koo za Walawi: ukoo wa Walibni; ukoo wa Wahebroni; ukoo wa Wamahli; ukoo wa Wamushi; ukoo wa wana wa Kora. (Kohathi alikuwa baba aliyemzaa Amramu;
59
jina la mke wa Amramu ni Yokebedi, naye pia alikuwa mzao wa Lawi, ambaye alizaliwa kwa Walawi nchini Misri. Alimzalia Amramu: Aroni, Mose na dada yao Miriamu.
60
Aroni alikuwa baba yake Nadabu na Abihu, Eleazari na Ithamari.
61
Lakini Nadabu na Abihu walikufa wakati walitoa sadaka mbele za Bwana kwa moto usioruhusiwa.)
62
Wanaume wote wa Walawi wa umri wa mwezi mmoja na zaidi walikuwa 23,000. Wao hawakuhesabiwa pamoja na Waisraeli wengine kwa sababu hawakupokea urithi miongoni mwao.
63
Hawa ndio walioorodheshwa na Mose na kuhani Eleazari wakati waliwahesabu Waisraeli kwenye nchi tambarare ya Moabu, kando ya Yordani ngʼambo ya Yeriko.
64
Hakuna hata mmoja wao aliyekuwa miongoni mwa wale waliohesabiwa na Mose na kuhani Aroni wakati waliwahesabu Waisraeli katika Jangwa la Sinai.
65
Kwa maana Bwana alikuwa amewaambia hao Waisraeli hakika wangekufa huko jangwani, wala hakuna mmoja wao aliyeachwa, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune na Yoshua mwana wa Nuni.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings