Hesabu 18:8-19
8
Kisha Bwana akamwambia Aroni, “Mimi mwenyewe nimekuweka kuwa mwangalizi wa sadaka zote zitakazotolewa kwangu; matoleo yote matakatifu Waisraeli wanayonipa ninakupa wewe na wanao kama sehemu yenu na fungu lenu la kawaida.
9
Mtachukua sehemu ya yale matoleo matakatifu sana ambayo hayateketezwi kwa moto. Kutoka kwa matoleo yote wanayoniletea kama sadaka takatifu sana, ziwe za nafaka, au za dhambi, au za makosa, sehemu ile itakuwa yako na wanao.
10
Mtaila kama kitu kilicho kitakatifu sana; kila mwanaume ataila. Ni lazima mtaiheshimu kama takatifu.
11
“Hiki pia ni chako: chochote kilichotengwa kutoka kwenye matoleo yote ya sadaka za kuinuliwa za Waisraeli. Ninakupa wewe haya, wana na binti zako kama sehemu yenu ya kawaida. Kila mmoja wa nyumba yako ambaye ni safi kwa taratibu za ibada anaweza kuyala.
12
“Ninawapa mafuta ya zeituni yaliyo bora kuliko yote, na divai mpya iliyo bora kuliko zote na nafaka wanazompa Bwana kama malimbuko katika mavuno yao.
13
Malimbuko yote ya nchi ambayo wanamletea Bwana yatakuwa yenu. Kila mmoja nyumbani kwako ambaye ni safi kwa taratibu za Ibada anaweza kula.
14
“Kila kitu katika Israeli ambacho kimetolewa kwa Bwana ni chenu.
15
Kila mzaliwa wa kwanza wa mwanadamu na wa mnyama, ambaye ametolewa kwa Bwana ni wenu. Lakini ni lazima mtamkomboa kila mwana mzaliwa wa kwanza na kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wasio safi.
16
Watakapokuwa na umri wa mwezi mmoja, ni lazima mtawakomboa kwa bei ya ukombozi iliyowekwa, kwa shekeli tano za fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, yenye uzito wa gera ishirini.
17
“Lakini kamwe usimkomboe mzaliwa wa kwanza wa maksai, kondoo au mbuzi; hawa ni watakatifu. Nyunyizia damu yao juu ya madhabahu na uchome mafuta yao kama sadaka itolewayo kwa moto, harufu nzuri inayompendeza Bwana.
18
Nyama zao zitakuwa chakula chenu, kama ilivyokuwa kidari cha kuinuliwa na paja la mguu wa kulia.
19
Chochote kitakachotengwa kutoka sadaka takatifu ambazo Waisraeli wanamtolea Bwana, ninakupa wewe, wanao na binti zako kama fungu lenu la kawaida. Ni Agano la milele la chumvi mbele za Bwana kwako na watoto wako.”
Settings