Hesabu 14:1-10
1
Usiku ule watu wote wa jumuiya walipaza sauti zao na kulia kwa sauti kuu.
2
Waisraeli wote wakanungʼunika dhidi ya Mose na Aroni, nalo kusanyiko lote wakawaambia, “Laiti tungekuwa tumefia humo nchi ya Misri! Au humu kwenye hili jangwa!
3
Kwa nini Bwana anatuleta katika nchi hii ili tufe kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watachukuliwa kama nyara. Je, isingekuwa bora kwetu kurudi Misri?”
4
Wakasemezana wao kwa wao, “Inatupasa kumchagua kiongozi na kurudi Misri.”
5
Ndipo Mose na Aroni wakaanguka kifudifudi mbele ya kusanyiko lote la Kiisraeli lililokusanyika hapo.
6
Yoshua mwana wa Nuni na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwa watu wale waliokwenda kuipeleleza nchi, wakararua nguo zao,
7
wakasema na kusanyiko lote la Kiisraeli, wakawaambia, “Nchi tuliyopita katikati yake na kuipeleleza ni nzuri sana sana.
8
Ikiwa Bwana anapendezwa nasi, atatuongoza kuingia katika nchi ile, nchi itiririkayo maziwa na asali, naye atatupa nchi hiyo.
9
Ila tu msimwasi Bwana. Wala msiwaogope watu wa nchi hiyo, kwa sababu tutawameza. Ulinzi wao umeondoka, lakini Bwana yupo pamoja nasi. Msiwaogope.”
10
Lakini kusanyiko lote likazungumza juu ya kuwapiga kwa mawe. Ndipo utukufu wa Bwana ukaonekana katika Hema la Kukutania kwa Waisraeli wote.
Settings