Nehemia 5:6-13
6
Niliposikia kilio chao na malalamiko haya, nilikasirika sana.
7
Nikayatafakari katika akili yangu, nikiwalaumu wakuu na maafisa. Nikawaambia, “Mnawaonea ndugu zenu kwa kuwatoza riba!” Basi nikaitisha mkutano mkubwa ili kuwashughulikia
8
na kusema: “Kulingana na uwezo wetu, tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi waliokuwa wameuzwa kwa watu wasioamini. Sasa mnawauza ndugu zenu, ili wauzwe tena kwetu!” Walinyamaza kimya, kwa sababu hawakupata chochote cha kusema.
9
Basi nikaendelea kusema, “Mnachokifanya si sawa. Je, haikuwapasa kutembea katika hofu ya Mungu wetu ili tuepukane na shutuma za adui zetu wasioamini?
10
Mimi na ndugu zangu na watu wangu tunawakopesha watu fedha na nafaka. Lakini jambo hili la kutoza riba likome!
11
Warudishieni mara moja mashamba yao, mashamba yao ya mizabibu, mashamba yao ya mizeituni, na nyumba zao, pia riba yao mnayowatoza na sehemu ya fungu la mia la fedha, nafaka, divai mpya na mafuta.”
12
Wakasema, “Tutawarudishia na hatutataka kitu chochote zaidi kutoka kwao. Tutafanya kama ulivyosema.” Kisha nikawaita makuhani na kuwafanya wakuu na maafisa kuapa kufanya kile walichoahidi.
13
Pia nikakungʼuta makunjo ya vazi langu na kusema, “Kila mtu ambaye hatatimiza ahadi hii, Mungu na amkungʼute hivi kutoka nyumba yake na katika mali zake. Basi mtu wa namna hiyo akungʼutiwe nje na aachwe bila kitu!” Waliposikia hili, mkutano wote ukasema, “Amen,” na wakamtukuza Bwana. Nao watu wakafanya kama walivyokuwa wameahidi.
Settings