Marko 9:11-23
11
Wakamuuliza, “Kwa nini walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?”
12
Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya yuaja kwanza ili kutengeneza mambo yote. Mbona basi imeandikwa kwamba Mwana wa Adamu ni lazima ateseke sana na kudharauliwa?
13
Lakini ninawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtendea walivyopenda, kama ilivyoandikwa kumhusu yeye.”
14
Walipowafikia wale wanafunzi wengine, wakawakuta wamezungukwa na umati mkubwa wa watu na baadhi ya walimu wa sheria wakibishana nao.
15
Mara wale watu walipomwona Yesu, wakastaajabu sana, wakamkimbilia ili kumsalimu.
16
Akawauliza wanafunzi wake, “Mnabishana nao kuhusu nini?”
17
Mtu mmoja miongoni mwa ule umati wa watu akajibu, “Mwalimu, nilimleta kwako mwanangu ambaye ana pepo mchafu anayemfanya asiweze kuongea.
18
Kila mara huyo pepo mchafu ampagaapo mwanangu, humwangusha chini na kumfanya atokwe povu mdomoni na kusaga meno, kisha mwili wake hukauka. Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”
19
Yesu akawaambia, “Enyi kizazi kisicho na imani! Nitakuwa pamoja nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana kwangu.”
20
Nao wakamleta yule mvulana. Yule pepo mchafu alipomwona Yesu, mara akamtia yule mvulana kifafa, akaanguka, akagaagaa chini huku akitokwa na povu kinywani.
21
Yesu akamuuliza baba yake, “Mwanao amekuwa katika hali hii tangu lini?” Akamjibu, “Tangu utoto wake.
22
Mara kwa mara huyo pepo mchafu amekuwa akimwangusha kwenye moto au kwenye maji ili kumwangamiza. Lakini kama unaweza kufanya jambo lolote, tafadhali tuhurumie utusaidie.”
23
Yesu akamwambia, “Kama ukiweza kuamini, yote yawezekana kwake yeye aaminiye.”
Settings