Marko 15:15-22
15
Pilato, akitaka kuuridhisha ule umati wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
16
Askari wakampeleka Yesu hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio, wakakusanya kikosi kizima cha askari.
17
Wakamvalisha Yesu joho la zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani.
18
Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!”
19
Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki.
20
Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe.
21
Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Aleksanda na Rufo, alikuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shamba, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.
22
Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa).
Settings