Walawi 22:1-16
1
Bwana akamwambia Mose,
2
“Mwambie Aroni na wanawe kushughulikia kwa uangalifu sadaka takatifu Waisraeli wanazoziweka wakfu kwangu, ili wasilinajisi Jina langu takatifu. Mimi ndimi Bwana.
3
“Waambie: ‘Katika vizazi vijavyo, ikiwa yeyote wa wazao wako ni najisi kwa taratibu za kiibada, naye akakaribia sadaka takatifu zile Waisraeli wanazoweka wakfu kwa Bwana, mtu huyo lazima akatiliwe mbali na uso wangu. Mimi ndimi Bwana.
4
“ ‘Ikiwa mzao wa Aroni ana ugonjwa wa ngozi unaoambukiza au anatokwa na usaha mwilini, hawezi kula sadaka takatifu mpaka atakasike. Pia atakuwa najisi ikiwa atagusa kitu chochote kilicho najisi kwa kugusa maiti au mtu aliyetokwa na shahawa,
5
au ikiwa atagusa kitu chochote kitambaacho kimfanyacho mtu najisi, au mtu yeyote awezaye kumtia unajisi, hata unajisi uwe gani.
6
Mtu anayegusa kitu chochote cha aina hiyo atakuwa najisi mpaka jioni. Kamwe hatakula sadaka yoyote takatifu mpaka yeye mwenyewe awe ameoga kwa maji.
7
Wakati jua linapotua, atakuwa safi, na baadaye anaweza kula sadaka takatifu, kwa kuwa ni vyakula vyake.
8
Kamwe asile nyama ya mzoga wala iliyoraruliwa na wanyama pori, naye akatiwa unajisi kwa hilo. Mimi ndimi Bwana.
9
“ ‘Makuhani lazima washike maagizo yangu ili wasiwe na hatia, wakafa kwa kuyadharau. Mimi ndimi Bwana ninayewafanya watakatifu.
10
“ ‘Hakuna mtu yeyote asiye wa jamaa ya kuhani anayeruhusiwa kula sadaka takatifu, hata mgeni wa kuhani au mfanyakazi wake haruhusiwi kuila.
11
Lakini ikiwa kuhani amenunua mtumwa kwa fedha, au mtumwa amezaliwa katika nyumba ya kuhani huyo, mtumwa huyo aweza kula chakula cha huyo kuhani.
12
Ikiwa binti wa kuhani ameolewa na mtu asiye kuhani, binti huyo haruhusiwi kula chochote cha matoleo matakatifu.
13
Lakini ikiwa binti wa kuhani amekuwa mjane au amepewa talaka, naye hana watoto, na akarudi kuishi na jamaa ya baba yake kama wakati wa usichana wake, binti huyo anaweza kula chakula cha baba yake. Hata hivyo, mtu asiyeruhusiwa hawezi kula chochote katika chakula hiki.
14
“ ‘Ikiwa mtu yeyote amekula sadaka takatifu kwa makosa, lazima atoe malipo ya sadaka hiyo kwa kuhani na kuongeza sehemu ya tano ya thamani ya sadaka hiyo.
15
Kamwe makuhani wasiinajisi sadaka takatifu ambayo Waisraeli wameitoa kwa Bwana
16
kwa kuwaruhusu kuzila sadaka hizo takatifu, na hivyo kuwaletea hatia ya kudaiwa malipo. Mimi ndimi Bwana niwafanyaye watakatifu.’ ”
Settings