Yoshua 23:1-9
1
Baada ya muda mrefu kupita, naye Bwana akawa amewapa Israeli pumziko mbele ya adui zao wote waliowazunguka, Yoshua, wakati huo akiwa mzee na umri ukiwa umeendelea sana,
2
akawaita Israeli wote, wazee wao, viongozi, waamuzi na maafisa Yoshua akawaambia: “Mimi ni mzee na umri wangu umeendelea sana.
3
Ninyi wenyewe mmeona kila kitu Bwana Mungu wenu, alichowatendea mataifa haya yote kwa ajili yenu. Ilikuwa ni Bwana Mungu wenu aliyewapigania.
4
Kumbukeni jinsi nilivyowagawia kama urithi kwa makabila yenu yote nchi ya mataifa yaliyobaki, yaani mataifa niliyowashinda, kati ya Mto Yordani na Bahari kuu upande wa magharibi.
5
Bwana Mungu wenu mwenyewe atawaondoa watoke mbele yenu. Atawafukuza mbele yenu, nanyi mtamiliki nchi yao, kama vile Bwana Mungu wenu alivyowaahidi.
6
“Kuweni hodari sana, kuweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika kitabu cha Sheria ya Mose, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto.
7
Msishirikiane na mataifa yaliyobakia katikati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia.
8
Bali mtashikamana kwa uthabiti na Bwana, Mungu wenu, kama vile ambavyo mmefanya mpaka sasa.
9
“Bwana amewafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu, mpaka siku ya leo hakuna yeyote aliyeweza kusimama mbele yenu.
Settings