Yohana 8:12-20
12
Kisha Yesu akasema nao tena akawaambia, “Mimi ni nuru ya ulimwengu. Mtu yeyote akinifuata hatatembea gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.”
13
Mafarisayo wakamwambia, “Ushuhuda wako haukubaliki kwa kuwa unajishuhudia mwenyewe.”
14
Yesu akawajibu, “Hata kama najishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu ni kweli kwa sababu najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.
15
Ninyi mnahukumu kwa kufuata vipimo vya kibinadamu, mimi simhukumu mtu yeyote.
16
Lakini hata kama nikihukumu, uamuzi wangu ni sahihi kwa sababu sitoi hukumu yangu peke yangu, bali niko pamoja na Baba, aliyenituma.
17
Imeandikwa katika Sheria yenu kwamba, ushahidi wa watu wawili ni thabiti.
18
Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma hunishuhudia.”
19
Ndipo wakamuuliza, “Huyo Baba yako yuko wapi?” Yesu akawajibu, “Ninyi hamnifahamu mimi ni nani, wala hammfahamu Baba yangu. Kama mngenifahamu mimi, mngemfahamu na Baba yangu.”
20
Yesu alisema maneno haya alipokuwa akifundisha katika chumba cha hazina Hekaluni. Lakini hakuna mtu aliyemkamata kwa kuwa saa yake ilikuwa haijawadia.
Settings