Skip to content
Yeremia 5:4-17

Yeremia 5:4-17

4
Ndipo nikasema, “Hawa ni maskini tu; wao ni wapumbavu, kwa maana hawaijui njia ya Bwana, sheria ya Mungu wao.
5
Kwa hiyo nitakwenda kwa viongozi na kuzungumza nao, hakika wao wanaijua njia ya Bwana, sheria ya Mungu wao.” Lakini kwa nia moja nao pia walikuwa wameivunja nira na kuvivunja vifungo.
6
Kwa hiyo simba kutoka mwituni atawashambulia, mbwa mwitu kutoka jangwani atawaangamiza, chui atawavizia karibu na miji yao, ili kumrarua vipande vipande yeyote atakayethubutu kutoka nje, kwa maana maasi yao ni makubwa, na kukengeuka kwao kumekuwa ni kwingi.
7
“Kwa nini niwasamehe? Watoto wenu wameniacha na kuapa kwa miungu ambayo si miungu. Niliwapatia mahitaji yao yote, lakini bado wamefanya uzinzi na kusongana katika nyumba za makahaba.
8
Wamelishwa vizuri, kama farasi waume wenye tamaa nyingi, kila mmoja akimlilia mke wa mwanaume mwingine.
9
Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya hili?” asema Bwana. “Je, nisijilipizie kisasi juu ya taifa kama hili?
10
“Piteni katika mashamba yake ya mizabibu na kuyaharibu, lakini msiangamize kabisa. Pogoeni matawi yake, kwa kuwa watu hawa sio wa Bwana.
11
Nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda wamekuwa si waaminifu kwangu kamwe,” asema Bwana.
12
Wamedanganya kuhusu Bwana. Wamesema, “Yeye hatafanya jambo lolote! Hakuna dhara litakalotupata; kamwe hatutaona upanga wala njaa.
13
Manabii ni upepo tu, wala neno halimo ndani yao, kwa hiyo hayo wayasemayo na yatendeke kwao.”
14
Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote: “Kwa sababu watu hawa wamesema maneno haya, nitayafanya maneno yangu vinywani mwenu kuwa moto, na watu hawa wawe kuni zinazoliwa na huo moto.
15
Ee nyumba ya Israeli,” asema Bwana, “Ninaleta taifa toka mbali dhidi yako, taifa la kale na linaloendelea kudumu, taifa ambalo lugha yao huijui, wala msemo wao huwezi kuuelewa.
16
Podo zao ni kama kaburi lililo wazi, wote ni mashujaa hodari wa vita.
17
Watayaangamiza mazao yenu na chakula chenu, wataangamiza wana wenu na mabinti zenu; wataangamiza makundi yenu ya kondoo na ya ngʼombe, wataangamiza mizabibu yenu na mitini yenu. Kwa upanga wataangamiza miji yenye maboma mliyoitumainia.

Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.

Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options