Isaya 29:1-8
1
Ole wako, wewe Arieli, Arieli, mji alimokaa Daudi! Ongezeni mwaka kwa mwaka, na mzunguko wa sikukuu zenu uendelee.
2
Hata hivyo nitauzunguka Arieli kwa jeshi, utalia na kuomboleza, utakuwa kwangu kama mahali pa kuwashia moto madhabahuni.
3
Nitapiga kambi pande zote dhidi yako, nitakuzunguka kwa minara na kupanga mazingirwa yangu dhidi yako.
4
Utakaposhushwa, utanena kutoka ardhini, utamumunya maneno yako kutoka mavumbini. Sauti yako itatoka katika nchi kama vile ya mzimu, utanongʼona maneno yako toka mavumbini.
5
Lakini adui zako wengi watakuwa kama vumbi laini, kundi la wakatili watakuwa kama makapi yapeperushwayo. Naam, ghafula, mara moja,
6
Bwana Mwenye Nguvu Zote atakuja na ngurumo, tetemeko la ardhi, na kwa sauti kuu, atakuja na dhoruba, tufani na miali ya moto iteketezayo.
7
Kisha makundi ya mataifa yote yale yapiganayo dhidi ya Arieli, yale yanayomshambulia yeye na ngome zake, na kumzunguka kwa jeshi, watakuwa kama ilivyo ndoto, kama maono wakati wa usiku:
8
kama vile mtu aliye na njaa aotavyo kuwa anakula, lakini huamka, bado njaa yake ingalipo, kama vile mtu mwenye kiu aotavyo kuwa anakunywa maji, lakini huamka akiwa anazimia, akiwa bado angali ana kiu. Hivyo ndivyo itakavyokuwa kwa makundi yote ya mataifa yanayopigana dhidi ya Mlima Sayuni.
Settings