Isaya 1:21-31
21
Tazama jinsi mji uliokuwa mwaminifu umekuwa kahaba! Mwanzoni ulikuwa umejaa unyofu, haki ilikuwa inakaa ndani yake, lakini sasa ni wauaji!
22
Fedha yenu imekuwa takataka, divai yenu nzuri imechanganywa na maji.
23
Watawala wenu ni waasi, rafiki wa wevi, wote wanapenda rushwa na kukimbilia hongo. Hawatetei yatima, shauri la mjane haliletwi mbele yao lisikilizwe.
24
Kwa hiyo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mwenye Nguvu wa Israeli, asema hivi: “Lo, nitapata faraja kutoka kwa adui zangu na kujilipizia kisasi juu ya watesi wangu.
25
Nitauelekeza mkono wangu dhidi yenu, nitawasafisha takataka zenu zote na kuwaondolea unajisi wenu wote.
26
Nitawarudishia waamuzi wenu kama ilivyokuwa siku za zamani, nao washauri wenu kama ilivyokuwa mwanzoni. Baadaye utaitwa, Mji wa Haki, Mji Mwaminifu.”
27
Sayuni itakombolewa kwa haki, wale waliomo ndani yake waliotubu kwa uaminifu.
28
Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa, nao wanaomwacha Bwana wataangamia.
29
“Mtaaibika kwa sababu ya hiyo mialoni ambayo mlifurahia, mtafadhaika kwa sababu ya bustani mlizozichagua.
30
Mtakuwa kama mwaloni wenye majani yanayonyauka, kama bustani isiyokuwa na maji.
31
Mtu mwenye nguvu atatoweka kama majani makavu yawakayo moto, na kazi yake kama cheche ya moto; vyote vitaungua pamoja, wala hakuna wa kuuzima huo moto.”
Settings