Isaya 1:2-20
2
Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia! Kwa maana Bwana amesema: “Nimewalisha watoto na kuwalea, lakini wameniasi mimi.
3
Ngʼombe anamjua bwana wake, naye punda anajua hori la mmiliki wake, lakini Israeli hajui, watu wangu hawaelewi.”
4
Lo! Taifa lenye dhambi, watu waliolemewa na uovu, uzao wa watenda mabaya, watoto waliozoelea upotovu! Wamemwacha Bwana, Wamemkataa kwa dharau yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli na kumgeuzia kisogo.
5
Kwa nini mzidi kupigwa? Kwa nini kudumu katika uasi? Kichwa chako chote kimejeruhiwa, moyo wako wote ni mgonjwa.
6
Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako hakuna uzima: ni majeraha matupu na makovu na vidonda vitokavyo damu, havikusafishwa au kufungwa wala kulainishwa kwa mafuta.
7
Nchi yenu imekuwa ukiwa, miji yenu imeteketezwa kwa moto; nchi yenu imeachwa tupu na wageni mbele ya macho yenu, imeharibiwa kama vile imepinduliwa na wageni.
8
Binti Sayuni ameachwa kama kipenu katika shamba la mizabibu, kama kibanda katika shamba la matikitimaji, kama mji uliohusuriwa.
9
Kama Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote asingelituachia walionusurika, tungelikuwa kama Sodoma, tungelifanana na Gomora.
10
Sikieni neno la Bwana, ninyi watawala wa Sodoma; sikilizeni sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora!
11
Bwana anasema, “Wingi wa sadaka zenu, ni kitu gani kwangu? Ninazo sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi, za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona. Sipendezwi na damu za mafahali wala za wana-kondoo na mbuzi.
12
Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu, ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo, huku kuzikanyaga nyua zangu?
13
Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana! Uvumba wenu ni chukizo kwangu. Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada: siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.
14
Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa: moyo wangu unazichukia. Zimekuwa mzigo kwangu, nimechoka kuzivumilia.
15
Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi, nitaficha macho yangu nisiwaone; hata mkiomba maombi mengi sitasikiliza. Mikono yenu imejaa damu;
16
jiosheni na mkajitakase. Yaondoeni matendo yenu maovu mbele zangu! Acheni kutenda mabaya,
17
jifunzeni kutenda mema! Tafuteni haki, watieni moyo walioonewa. Teteeni shauri la yatima, wateteeni wajane.
18
“Njooni basi tuhojiane,” asema Bwana. “Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu, zitakuwa nyeupe kama theluji; ingawa ni nyekundu sana kama damu, zitakuwa nyeupe kama sufu.
19
Kama mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi,
20
lakini kama mkikataa na kuasi, mtaangamizwa kwa upanga.” Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena.
Settings